Friday, November 20, 2015

BUNDESLIGA: LEO HII USIKU BORUSSIA DORTMUND UWANJANI! KUIKARIBIA BAYERN NA KUFUTA GUNDU LA MIAKA 9!

LEO Usiku Borussia Dortmund wanaweza kuwakaribia Vinara wa Bundesliga Bayern Munich na kuwa Pointi 2 nyuma yao ikiwa safari yao huko kwa Hamburg SV itakuwa na mafanikio kwenye Mechi pekee ya Bundesliga hii Leo ambayo pia imewekewa ulinzi kumkali kutokana na hali tete ya usalama huko Barani Ulaya.
Baada ya Watu 129 kuuawa huko Paris Ijumaa iliyopita kutokana na mashambulio ya magaidi na ile Mechi ya Kirafiki kati ya Timu za Taifa za Germany na Netherlands iliyokuwa ichezwe Jumanne huko Hannover kufutwa kutokana na tishio la bomu, Mechi zote za Bundesliga Wikiendi hii zitachezwa chini ya ulinzi mkali.
Klabu huko Germany zimetaka Mashabiki wafike Uwanjani mapema kwa sababu wanaweza kuchelewa kutokana na ukaguzi wa nje na ndani ya Viwanja.

Dortmund wanatinga kwenye Mechi ya hii Leo wakisaka ushindi wao wa 5 mfululizo kwenye Bundesliga ambao utawafikisha Pointi 2 tu nyuma ya Vinara Bayern Munich ambao wanacheza Ugenini Jumamosi na Schalke.
Hivi sasa Bayern wanaongoza Ligi wakiwa na Pointi 34 na Nafasi ya Pili ni Dortmund wakiwa na Pointi 29.

Dortmund, chini ya Kocha Thomas Tuchel, wanatarajiwa kuwa nae tena Marco Reus ambae aliumia Novemba 4 ili kujumuika na kina Gonzalo Castro, Shinji Kagawa, Henrikh Mkhitaryan na Pierre-Emerick Aubameyang huko Ugenini Hamburg ambako wameshinda mara 1 tu katika Miaka 9.

Hapo Kesho Jumamosi, Mabingwa Bayern wanasafiri kwenda kucheza huko Schalke kuendeleza mwanzo wa mzuri kwenye Bundesliga ambako Wameshinda Mechi 11 na Sare 1 katika Mechi zao 12 Msimu huu.