Friday, November 20, 2015

MENEJA JOSE MOURINHO APANIA KULETA WAPYA CHELSEA KWENYE DIRISHA DOGO!

Jose Mourinho anategemea vakesheni ya Wiki 2 ya Ligi Kuu England kupisha Mechi za Kitaifa itainufaisha Timu yake Chelsea kupindua mlolongo wa vipigo kwa Jumamosi kuifunga Norwich City Uwanjani Stamford Bridge katika Mechi ya Ligi.
Kabla Ligi Kuu England kusimama, Chelsea ilifungwa na Stoke City na hicho kulikuwa kipigo chao cha 3 mfululizo kwenye Ligi kilichowabwaga hadi Nafasi ya 16 wakiwa Pointi 1 nyuma ya wapinzani wao wa Jumamosi Norwich City na Pointi 3 juu ya zile Timu 3 za mkiani.
Kipigo hicho, bila shaka, kilizidisha presha kwa Mourinho na labda hizi Wiki 2 za mapumziko kimempa muda wa kutafakari kwa undani nini tatizo la Timu yake.
Kwa Wachambuzi wengi huko England tatizo la Chelsea ni kuwa wengi wa Wachezaji wao wanacheza chini ya kiwango tofauti na Msimu uliopita walipotwaa Ubingwa.

Licha ya kufungwa na Stoke katika Mechi yao iliyopita, Mourinho alidai Kikosi chake kimeongeza kiwango cha uchezaji lakini hilo hakuna atakaelijali ikiwa Timu haishindi. Njia pekee kwa Mourinho ni kutafuta namna ya kupata ushindi na hilo inabidi lianzie kwa Staa wao Eden Hazard, ambae Msimu uliopita alizoa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka, lakini safari hii ameporomoka vibaya.
Pengine habari njema kwa Mourinho katika wakati wake mgumu ni kupona kwa Kipa wake Nambari Wani Thibaut Courtois ambae amerejea mazoezini lakini Asmir Begovic ndie ataeikabili Norwich.
Norwich, licha ya kuwa Pointi 1 juu ya Chelsea, walitoka kwenye wimbi la vipigo vya Mechi 4 za Ligi na kushinda Mechi yao ya mwisho walipoibwaga Swansea City.