Sunday, December 20, 2015

ANCELOTTI KUCHUKUA NAFASI YA PEP GUARDIOLA BAYERN MUNICH


MABINGWA wa Bundesliga huko Germany, Bayern Munich, wametangaza kuwa Kocha wa zamani wa Real Madrid na Chelsea, Carlo Ancelotti, ndie atakuwa Kocha wao mpya kwa Msimu ujao.
Kocha wa sasa, Pep Guardiola, anatarajiwa kujiunga na Manchester City ingawa hili bado kuthibitishwa na anabaki pia kuhusishwa na Man United na Chelsea.
Hata hivyo, Kocha huyo wa zamani wa Barcelona mwenye Miaka 44 ana nafasi kubwa kutua Etihad hasa kutokana na urafiki wake wa karibu na Mkurugenzi wa Soka wa CitY Txiki Begiristain pamoja na Mtendaji Mkuu Ferran Soriano, Watu ambao alikuwa nao Barcelona.
Mwezi Agosti, Man City ilimwongezea Meneja wao wa sasa, Manuel Pellegrini, Mkataba wa Mwaka mmoja zaidi hadi Juni 2017 lakini hilo linaonekana si tatizo kwa Guardiola kumbadili.
Guardiola alijiunga na Bayern Munich Mwaka 2013 na kutwaa Ubingwa wa Bundesliga kila Msimu na safari hii pia yuko njiani kuutwaa kwa mara ya 3 mfululizo.
Akiwa na Barcelona, kwa Miaka Minne, Guardiola aliweza kuiongoza kutwaa La Liga mara 3 na UEFA CHAMPIONS LIGI mara 1.
Carlo Ancelotti, ambae amekuwa hana kibarua tangu Msimu uliopita alipoondolewa Real Madrid, amesaini Mkataba wa Miaka Mitatu na Bayern Munich.