Wednesday, December 2, 2015

CHELSEA KUTANUA WAKE STAMFORD BRIDGE

Chelsea imewasilisha maombi ya mpango wao wa kuupanua Uwanja wa Stamford Bridge ili upakie Mashabiki 60,000 ambao utahusisha kuvunjwa Majengo ya Jirani.
Maombi hayo yatachunguzwa na Manispaa ya London Borough of Hammersmith and Fulham ambayo pia imekaribisha maoni toka kwa Wananchi na Wadau wengine ambao watatakiwa kutoa maoni yao au pingamizi zao kabla ya Tarehe 8 Januari 2016.
Chelsea walianza kucheza Uwanjani Stamford Bridge tangu 1905 ambako mara ya mwisho kukarabatiwa na kupanuliwa ni katika Miaka ya 1990 na kuufanya upakie Watu 42,000.
Lakini idadi hiyo ni ndogo mno ukilinganisha na Wapinzani wake wa Ligi Kuu England Manchester United wenye Old Trafford inayochukua Watu 76,000, Arsenal na Emirates yao yenye uwezo wa Mashabiki 60,000 na Etihad ya Manchester City inayopakia Watu 55,000.
Awali, Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, alitafakari kuhama kabisa Stamford Bridge baada kupata vikwazo vya upanuzi wake lakini pia akakwama kupata eneo jipya jingine ndani ya Jiji la London.