Monday, December 21, 2015

JOSE MOURINHO NJIA NYEUPE KUTUA OLD TRAFFORD!


WAKATI uvumi na tetesi kubwa zikipamba anga za England kuhusu kutimuliwa kwa Meneja wa sasa wa Manchester United, Louis van Gaal, kutokana na mwendo mbovu, nani atamrithi kimekuwa kitendawili kikubwa.
Wapo Wachambuzi wanaomtaka Meneja Msaidizi wa Man United, Ryan Giggs, apewe kiti hicho, wapo wale ambao wanadai Jose Mourinho, aliefukuzwa Chelsea Wiki iliyopita, tayari ameshasaini Mkataba na Man United.
Mmoja wa wanaompigia debe Giggs ni Steve Round aliewahi kuwa Meneja Msaidizi wa Man United chini ya himaya ya David Moyes ambapo Giggs alikuwa mmoja wa Makocha.
Round amedai Giggs sasa ana uzoefu na anastahili kupewa fursa hii.
Lakini wapo Wachambuzi wengi wanaodai Klabu kubwa Duniani kama Man United inahitaji Meneja mzoefu wa rika la Jose Mourinho.
Kuhusishwa kwa Mourinho na Man United si kitu kigeni kwani Mreno huyo mwenye Miaka 52 ashawahi kuhusishwa na kujiunga wakati ule Sir Alex Ferguson alipostaafu Mwaka 2013 lakini bahati mbaya alikuwa ashasaini Mkataba na Chelsea.

Kwa sasa Mourinho yupo huru na mwenyewe ashatangaza yuko tayari kurejea kibaruani mara moja na huu, kwa Wachambuzi, ni wakati muafaka kwa yeye kutua Old Trafford hasa kwa vile Desemba 28 Chelsea watatua Old Trafford kucheza na Man United Mechi ya Ligi Kuu England.
Lakini pia, mwishoni mwa Msimu yupo huru Pep Guardiola baada ya kutangaza kuachana na Bayern Munich mwishoni mwa Msimu huu na tayari Mabingwa hao wa Bundesliga washamteua Carlo Ancelotti kuwaongoza.
Lakini huyu inaaminika mwelekeo wake ni kwenda Man City kuungana tena na Marafiki zake aliokuwa nao Barcelona, Tziki Begiristain na Ferran Soriano, ambao sasa ni Maafisa Waandamizi wakubwa huko Man City.
Kama ilivyo kawaida ya Klabu ya Man United hamna tamko lolote walilotoa hadi sasa.