Tuesday, December 29, 2015

KIWANGO SAFI CHA MAN UNITED KWA KUTOKA SARE YA 0-0 NA CHELSEA, BODI YA MAN UNITED YAKUBALIANA NA VAN GAAL KUENDELEA NAE!

MARA baada ya Jumatatu Usiku kutoka Sare 0-0 na Mabingwa Watetezi Chelsea Uwanjani Old Trafford na kusitisha wimbi la kufungwa Mechi 4 mfululizo, Meneja wa Manchester United Louis van Gaal aliibuka na kutamba hana mipango ya kujiuzulu.
Baada ya kuchapwa 2-0 na Stoke City Siku ya Boksing Dei, Man United waliibuka na kusakata Soka safi na kustahili kuifunga Chelsea lakini, kama kawaida, umaliziaji uliwaangusha.
Hali hiyo ilimfanya Louis van Gaal apige ‘abauti tani’ na kudai Wachezaji wake wamempa sababu ya kutojiuzulu tofauti na alivyodokeza huko Britannia Stadium mara baada ya kufungwa na Stoke. Jana Van Gaal alisema: “Wachezaji wakicheza namna ile hasa wakati huu wa presha kubwa, hamna sababu ya mimi kujiuzulu. Labda Vyombo vya Habari wanataka hivyo, ila sitafanya.”
Wakati huo huo, Mchambuzi wa Soka anaeaminika huko England, Andy Gray, Mchezaji wa zamani wa Scotland aliechezea Klabu kadhaa huko England, amedai Man United hawana uchu wa kumwajiri Jose Mourinho kama Meneja.
Mourinho, ambae alitimuliwa na Chelsea Wiki iliyokwisha, amekuwa akitajwa na wengi kuwa atachukua wadhifa wa Van Gaal.

Jumatatu, nje ya Old Trafford, kwenye Mechi na Chelsea, Wachuuzi walikuwa wakitembeza bidhaa kadhaa zikiwa na Nembo ya Man United na Jina la Jose Mourinho wakimpigia debe kuwa Meneja wa Man United.
Lakini Andy Gray anaamini Bodi ya Man United bado inamsapoti Van Gaal na haimtaki Mourinho ambae wanaona hulka yake haiendani na utamaduni wa Man United.