Tuesday, December 29, 2015

MENEJA WA SPURS MAURICIO POCHETTINO ASEMA UBINGWA HAUNA TIMU MPAKA SASA HATA SPURS INAWEZA KUUTWAA UBINGWA!

BAADA ya kuwachapa Watford Bao 2-1 Jumatatu Usiku na kushika Nafasi ya 3 ya Ligi Kuu England, Meneja wa Tottenham Hotspur Mauricio Pochettino amedai Timu yake inaweza kutwaa Ubingwa Msimu huu.
Spurs, wenye Pointi 38 baada ya Mechi 19, wako Pointi 4 nyuma ya Vinara Arsenal na Pointi 3 nyuma ya Timu ya Pili Leicester City.

Akiongea na Wanahabari, Pochettino alisema: “Nadhani namba zinasema Ubingwa unawezekana. Kitu muhimu ni sisi kuendelea na juhudi kubwa.”
Pochettino, Raia wa Argentina, amesisitiza Kikosi chake kina Wachezaji wachanga na hivyo kinapaswa kufanya kazi kwa bidii zaidi.
Jumapili ijayo, Spurs watakuwa huko Goodison Park kucheza na Everton na kisha kuivaa Leicester City na Sunderland.
Pochettino amesisitiza: “Muhimu tusibweteke. Tuna Wachezaji wenye uerevu na wajanja ambao wako tayari kujifunza. Muhimu tuwe vile vile kama tulivyoanza Ligi.”
Tangu Ligi Kuu England ianzishwe, Tottenham hawajawahi kumaliza ndani ya 3 Bora na mara mbili, Msimu wa 2009/10 na ule wa 2011/12, walimaliza Nafasi ya 4.