Thursday, January 28, 2016

BRENDAN RODGERS AMTETEA LOUIS VAN GAAL, ASEMA WACHEZAJI NDIO WAKUTUPIWA MACHO!

MENEJA WA zamani wa Liverpool Brendan Rodgers amemtetea Louis van Gaal ambae ni Meneja wa Manchester United anaesakamwa huku Timu yake ikisuasua.
Van Gaal amelaumiwa mno kwa staili yake ya uchezaji na Wachezaji wa zamani wa Man United pamoja na Mashabiki wa Timu hiyo wameiita staili ya Mholanzi huyo kuwa ni ‘doro’, isiyovutia na iliyopooza mno.
Man United, waliosifika kwa kucheza Soka la Kishujaa la Mashambulizi mfululizo chini ya Meneja Lejendari Sir Alex Ferguson, wamefunga Bao 12 tu kwao Old Trafford Msimu huu katika Ligi Kuu England na Jumamosi iliyopita walipofungwa 1-0 na Southampton Uwanjani hapo walipiga Shuti 1 tu Golini katika Mechi hiyo licha ya kutawala na kumiliki Mpira sana kama ilivyo kawaida kwa Mechi zao nyingi Msimu huu.
Lakini Brendan Rodgers amemtetea Van Gaal na kuamini Soka bovu na lisilo la kuvutia wanalocheza Man United ni sababu ya Wachezaji alio nao na si Meneja huyo ambae ana rekodi nzuri ya Timu zilizocheza Soka safi na la kushambulia.

Rodgers amesema: “Si kweli Van Gaal anapanga Kikosi ili wapige Mashuti machache Golini. Huyu ni Mtu ambae yuko juu muda mrefu, anaelewa Soka na Mwaka 1995 aliijenga Ajax ambayo kila Mtu aliizungumzia Miaka nenda rudi. Ndio ilikuwa ni Soka la kumiliki Mpira lakini pia la kushambulia mno. Ni wazi alipokuwa Barcelona ilikuwa hivyo hivyo. Alienda Bayern Munich ilikuwa hivyo hivyo, kumiliki Mpira na kushambulia. Ukiingalia Man United na kuwatazama Wachezaji wake, je wanao Wachezaji wanaoweza kucheza Soka la kuvutia kama huko nyuma? Hiyo ndio sababu kubwa!”
Aliongeza: “Na hilo ndio jambo ambalo Wanahabari wanamshambulia nalo kila kukicha. Lakini huyu ni Mtu aliekuwa juu kwa muda mrefu sana. Ni ngumu kwake hapa lakini alijua nini atakuta Nchi hii.”
Brendan Rodgers yupo nje ya kazi tangu atimuliwe kama Meneja wa Liverpool Oktoba Mwaka Jana.
Alipohojiwa kama atakuwemo kwenye Listi ya wagombea Umeneja ikiwa Van Gaal ataondoka, Rodgers alicheka na kujibu: “Nadhani ukiwa Meneja Liverpool ile kazi ya Umeneja Manchester United inakuwa nje kwako!”