Monday, January 25, 2016

KLABU ZA MADRID ZAKWAMA, ZAIACHA BARCELONA IKITAMBA KILELENI!

VIGOGO wa Jiji la Madrid huko Spain, Real Madrid na Atletico Madrid, Jana wote walitoka Sare kwenye La Liga na kuwaacha Mabingwa Watetezi Barcelona wapete kileleni huku wakiwa na Mechi 1 mkononi.
Juzi Barca waliichapa Malaga 2-1 na kutwaa uongozi wa La Liga huku wakiwa wamecheza Mechi 1 pungufu.
Mapema Jana, Atletico Madrid, ikiwa kwao Vicente Calderon, ilitoka 0-0 na Sevilla waliocheza Mtu 10 kuanzia Dakika ya 61 baada ya Victor Machin Perez Vitolo kulambwa Kadi za Njano 2 na kutolewa kwa Kadi Nyekundu.
Huko Estadio Benito Villamarin hapo Jana, Real Madrid walinusurika kichapo kutoka kwa Real Betis baada ya Karim Benzema kuwaokoa aliposawazisha katika Dakika ya 71 na Mechi kwisha 1-1.
Real Betis, ambao hawajashinda katika Mechi zao 11 zilizopita, walifunga Bao lao Dakika ya 7 kupitia Alvaro Cejudo.
Kwenye Mechi hiyo, Cristiano Ronaldo, aliekuwa goigoi, alikosa Bao kadhaa akiungana na James Rodriguez aliekosa nafasi 2 za wazi.
Sare hii imemfanya Kocha mpya wa Real, Zinedine Zidane, aendelee na rekodi ya kutofungwa tangu atwae wadhifa huu mapema Mwezi huu kutoka kwa Rafa Benitez aliefukuzwa.
Barca sasa wako kileleni wakiwa na Pointi 48 kwa Mechi 20 wakifuata Atletico wenye Pointi 48 pia kwa Mechi 21, kisha Real Pointi 44 kwa Mechi 21 na wa 4 ni Villareal wenye Pointi 41 kwa Mechi 21.