Saturday, January 16, 2016

LIGI KUU VODACOM: KHAMISI KIIZA AIPA USHINDI SIMBA KUIUA MTIBWA BAO 1-0!

Kocha wa Simba, Jackson Mayanja akisalimiana na kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime
SIMBA imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam leo.
Pamoja na ushindi huo Simba imebaki kwenye nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 30 sawa na Yanga inayoshika nafasi ya pili, lakini Yanga ikiwa mbele kutokana na kuwa na mabao mengi ya kufunga.
Hiyo ni mara ya pili kwa Simba na Mtibwa kukutana katika kipindi cha wiki mbili kwani walikutana kwenye mchezo wa nusu fainali wa kombe la Mapinduzi na Mtibwa Sugar kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kwenye mchezo wa leo Simba ilikuwa bila ya kocha wake mkuu Dylan Kerr aliyefungashiwa virago kufuatia mwenendo mbaya wa timu hiyo, walipata bao lao mapema kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji Hamisi Kiiza dakika ya nne. Dakika ya 13 kiungo Justice Majavi alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia rafu kiungo wa Mtibwa Shiza Kichuya na dakika tatu baadae Kiiza alipoteza nafasi nzuri ya kufunga kwa shuti lake kupaa juu ya lango la Mtibwa.
Kwenye dakika ya 31 Simba walifanya mabadiliko kwa kumpumzisha winga Peter Mwalyanzi na kumuingiza Said Ndemla aliyechangamsha zaidi sehemu ya kiungo ya timu hiyo.
Dakika ya 47 Mtibwa Sugar walipoteza nafasi nzuri ya kusawazisha lakini kiungo wake aliye kwenye kiwango bora Shiza Kichuya alipiga mpira uliotoka pembeni ya lango la Simba.
Mtibwa Sugar walitawala kiasi sehemu ya kiungo na nusura wapate bao lakini shuti la beki wa kushoto wa timu hiyo Issa Rashidi kwenye dakika ya 54 kugonga mwamba na kuokolewa na mabeki wa Simba.
Timu zote zilifanya mabadiliko kwa Mtibwa Sugar kumpumzisha Mohamedi Ibrahim na kumuingiza Vicent Barnabas na Simba kumtoa Ibrahim Ajib aliyeumia na kumuingiza Danny Lyanga na kipa wa Simba Vicent Angban alionyeshwa kadi ya njano kwa kupoteza muda.

BAO la Dakika ya 5 la Hamisi Kiiza Leo limeipa Simba ushindi wa 1-0 walipocheza na Mtibwa Sugar katika Mechi ya Ligi Kuu Vodacom, VPL , kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Ushindi huu umezidi kuwachimbia Simba Nafasi ya 3 kwenye VPL sasa wakiwa na Pointi 30 kwa Mechi 14 wakiwa Pointi 3 nyuma ya Yanga na Pointi 5 nyuma ya Vinara huku Timu mbili hizo zikiwa zote zimecheza Mechi 13.
Baadae Usiku huu, huko Azam Complex, Chamazi, kwenye Viunga vya Jiji la Dar es Salaam, Azam FC wataingia dimbani kucheza na African Sports.
Jumapili, ndani ya Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, Mabingwa Watetezi Yanga watacheza na Ndanda FC.