Friday, January 8, 2016

LOUIS VAN GAAL: ‘SITISHIKI PEP GUARDIOLA KUJA ENGLAND!’

BOSI wa Manchester United Louis van Gaal amesema hatishiki na mipango ya Pep Guardiola kuja kuwa Meneja wa Klabu inayocheza Ligi Kuu England.
Guardiola, mwenye Miaka 44 na ambae sasa ni Meneja wa Bayern Munich ya Germany, ametangaza ataondoka huko Germany Mwezi Mei baada ya kudumu Misimu Mitatu na Mabingwa hao wa Germany.

Meneja huyo wa zamani wa Barcelona anahusishwa na kwenda Klabu za Manchester, Man United na Man City, pamoja pia na Chelsea na Arsenal za Jijini London.
Mwenyewe Guardiola ashaweka bayana kuwa kituo chake cha kazi kinachofuata ni Ligi Kuu England lakini amesema hajasaini popote na akisaini ni Klabu yenyewe ndio itatangaza.
Ujio huo haukumtisha Louis van Gaal ambae alipohojiwa kama ana wasiwasi kwa Guardiola kuchukua kibarua chake alijibu: “Yeye anataka kuja England, ni vizuri kwake. Mie ndio nafikia tamati ya maisha yangu ya kazi na hilo la Guardiola sijali, halinivutii!”

Van Gaal, mwenye Miaka 64, ana Mkataba na Man United hadi mwishoni mwa Msimu wa 2016/17 na sasa amepita kipindi kigumu cha Mechi 8 bila ushindi hadi wikiendi iliyopita walipoichapa Swansea City 2-1.
Jumamosi Man United wako Old Trafford kucheza na Sheffield United katika Mechi ya Raundi ya 3 ya FA CUP.