Sunday, January 31, 2016

MENEJA LOUIS VAN GAAL AWAASA MASHABIKI KUTOZOMEA TIMU, WAMZOMEE YEYE TU!

Kocha Mkuu wa Manchester United Louis van Gaal anatarajia wakati mwingine mgumu kwake Uwanjani Old Trafford wakati Jumanne Usiku Timu yake itakapocheza na Stoke City kwenye Ligi Kuu England.
Juzi Man United iliifunga Derby County 3-1 na kutinga Raundi ya 5 ya EMIRATES FA CUP na hiyo kupunguza presha kwa Van Gaal kufuatia kipigo cha 1-0 toka kwa Southampton ndani ya Old Trafford katika Mechi ya kabla ya hapo huku uchezaji wa Timu ukiamsha hasira za Mashabiki waliomzomea Van Gaal wakati wa Mechi na mwishoni mwake.
Licha ya kuifunga Derby, Van Gaal hana hakika na mapokezi ya Mashabiki ndani ya Old Trafford lakini amesema yeye hajali kuzomewa kwani kitu muhimu ni Mashabiki hao kuwa nyuma ya Wachezaji wake.

Van Gaal amesema: “Mimi si mpumbavu. Nina akili na siwezi kutabiri hali itakuwaje hapo Jumanne. Natarajia tutacheza kiwango kilekile cha Mechi na Derby lakini tunacheza na Stoke, ni mpinzani mwingine.”

Aliongeza: “Si muhimu wakinizomea mimi. Ni muhimu wakiwasapoti Wachezaji, ni jambo muhimu sana. Wachezaji ndio wenye kazi ngumu zaidi. Wao ndio hutoa matokeo dhidi ya upinzani wa Stoke. Hamna kisingizio. Ni muhimu wasapoti-hawa Mashabiki.”

Mwezi Desemba, Siku ya Boksing, huko Britannia Stadium, Stoke iliichapa Man United 2-0 kwenye Ligi na kuzusha presha kubwa ya kufukuzwa Van Gaal lakini vuguvugu hilo likatulia Siku 2 baadae baada ya kutoka Sare na Mabingwa wa England, Chelsea.

Kuhusu Stoke City, ambayo iko chini ya Mark Hughes, Mchezaji wa zamani wa Man United, Van Gaal ameeleza: “Napenda sana jinsi Stoke wanavyocheza. Niliwaona Wiki hii wakicheza na ni wazuri mno. Walistahili kuifunga Liverpool lakini hawakushinda. Hilo ni Soka, unaweza kufungwa. Stoke wana shepu nzuri na fomu nzuri. Wao ni Timu ambayo kila Timu kwenye Ligi Kuu hupata wakati mgumu kutoka kwao.”

Hivi sasa Man United wapo Nafasi ya 5 kwenye Ligi wakiwa Pointi 5 nyuma ya Tottenham ambao wako Nafasi ya 4, ambayo ndio ya mwisho kuchezea UEFA CHAMPIONS LIGI, na Pointi 10 nyuma ya Vinara Leicester City huku Mechi zikibaki 15.
Stoke City wao wako Nafasi ya 9 wakiwa Pointi 4 nyuma ya Man United.