Sunday, January 31, 2016

NAHODHA JOHN TERRY KUACHANA NA CHELSEA MWISHONI MWA MSIMU HUU 2015/2016.

WAKATI Kepteni wa Chelsea John Terry akitoboa Jana kuwa ataondoka Stamford Bridge mwishoni mwa Msimu huu baada ya kutopewa nyongeza ya Mkataba wake unaoisha wakati huo, Klabu imetoa Taarifa inayosisitiza kuwa Nahodha wao anaweza kubakia hapo.
Mara baada ya kuifunga MK Dons Jumapili na kutinga Raundi ya 5 ya EMIRATES FA CUP, Terry aliwaambia Wanahabari: “Hautakuwa mwisho mwema. Sitastaafu Chelsea na hili limenichukua Siku kadhaa kukubali hali hii. Ningependa sana kubaki hapa lakini Klabu ina mwelekeo tofauti!”
Lakini Klabu imetoa Taarifa inayosisitiza kuwa Nahodha wao anaweza kubakia hapo baada ya Msimu huu kwisha.

Chelsea bado haina Meneja wa kudumu baada ya kumfukuza Jose Mourinho na kumteua Guus Hiddink hadi mwishoni mwa Msimu na inaelekea Meneja wa kudumu ndie mwenye uamuzi wa kumbakisha Terry au la.

Msemaji wa Chelsea ameeleza: “John aliomba kukutana na Klabu kabla ya Wiki iliyopita. Katika Mkutano huo aliomba kujua uwezekano wa kuongezewa Mkataba baada ya Mkataba wa sasa kwisha. John alijulishwa kwa sasa hamna Dili mpya mezani ila hali inaweza kubadilika Miezi michache ijayo. Klabu inamuheshimu mno John na vyote alivyofanya kutupa mafanikio. Ni Mtumishi bora wa Chelsea na Kepteni murua na hivyo Klabu inaacha milango yote wazi.”
Tery alijiunga na Chelsea akiwa na Miaka 14 na ameichezea Mechi 696 na kufunga Mabao 66 katika Misimu 18 aliyochezea Kikosi cha Kwanza.


Mataji aliyotwaa Terry akiwa na Chelsea ni UEFA CHAMPIONS LIGI Mwaka 2012, Ubingwa wa Ligi Kuu England mara 4, FA CUP 5, Kombe la Ligi 3 na Mwaka 2013 kutwaa UEFA EUROPA LIGI.

Mwenyewe Terry amesisitiza bado ana hamu ya kucheza Soka la kiwango cha juu lakini hataichezea Klabu yeyote nyingine ya England akiondoka Chelsea.