Tuesday, January 5, 2016

UONGOZI WA REAL MADRID WAMTAMBULISHA ZINEDINE ZIDANE KUWA MENEJA WAKE LEO!

Zidane atambulishwa rasmi leo Real Madrid, Ni baada ya
Rafael Benitez kufukuzwa  Real Madrid baada ya Miezi 7 tu katika wadhifa wake na Lejendari Zinedine Zidane amepewa hatamu kwa Mkataba wa Miaka Miwili na Nusu.
Zidane, mwenye Miaka 43, alikuwa Kocha Mkuu wa Timu B ya Real Madrid, iitwayo Castilla, huku Wanawe wa Kiume Wanne wakizichezea Timu za Vijana za Real.
Zidane, ambae alitwaa Kombe la Dunia akiwa Mchezaji na Nchi yake France Mwaka 1998, aliwahi kuwa Mchezaji wa Real kuanzia 2001 aliponunuliwa kwa Rekodi ya Dunia wakati huo kutoka Juventus na kucheza hadi 2006.

Akiongea mara baada ya kutambulishwa, Zidane alisema: “Nitatoa moyo na roho yangu kwa kazi hii ili kila kitu kiende sawa!”

Tangu atue Real, Benitez amekuwa si kipenzi cha Mashabiki wa Klabu hiyo, na kutandikwa 4-0 kwenye El Clasico Mwezi Novemba na Mahasimu wao Barcelona hakukumsaidia hata kidogo.

Pia kutupwa nje ya Copa del Rey baada ya kumchezesha Mchezaji asiestahili katika Mechi na Cadiz kumechochea chuki dhidi yake.

Hali hiyo ilifanya kuwepo minong’ono ya kila mara kuwa Wachezaji wa Real hawana raha na Benitez na wana mgomo baridi dhidi yake.

Wiki iliyopita Benitez aliwatuhumu Wanahabari kwa kuendesha kampeni kumpinga yeye, Klabu na Rais wao Florentino Per├ęz.

Juzi Real ilitoka Sare 2-2 na Kikosi cha Gary Neville, Mchezaji wa zamani wa Man United ambae sasa anaifundisha Valencia, iliyotoka 2-2 na Real Uwanjani Mestalla katika Mechi ya La Liga, Sare ambayo imewaacha Vigogo hao Nafasi ya 3 wakiwa Pointi 4 nyuma ya Vinara Atletico Madrid, na kuleta presha kubwa kwa Rafa Benitez.

Zidane anakuwa Kocha wa 11 wa Real chini ya Rais Florentino Perez kwenye himaya yake ya Miaka 12 katika Vipindi viwili.

Mechi ya kwanza kwa Zidane kama Kocha Mkuu wa Real itakuwa Jumamosi Uwanjani Santiago Bernabeu wakati Real ikicheza na Deportivo la Coruna kwenye La Liga.