Saturday, January 30, 2016

YASSODA AWAPA SOMO WAHITIMU MAKOCHA WANAWAKE


MKURUGENZI Msaidizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Yassoda amewataka makocha wanawake kuwa chachu ya maendeleo ya soka lao baada ya kuhitimu mafunzo.
Yassoda aliyasema hayo wakati akifunga kozi ya ukocha wa wanawake ngazi ya juu iliyoandaliwa na TFF kwa kushirikiana na FIFA, iliyofanyika Karume kwa siku tano
Akizungumza wakati wa kufunga kozi hiyo, Yassoda amesema anaishukuru TFF/FIFA kwa kuona wanawake wanapata nafasi ya kushiriki kozi mbalimbali, ikiwemo kozi hiyo ya ukocha kwa ngazi ya juu.
“Jamani kilio na mwenyewe, siyo wewe macho makavu halafu utegemee waombelezaji walie, hivyo mkafanye kazi ya kufundisha ili baadae tuwe na makocha wa kusimamia timu zetu za taifa za wanawake,” alisema Yassoda
Pia Yassoda amewataka washiriki kuhamasisha wanawake wengi kuupenda mpira wa miguu na kuzalisha vipaji vya wachezaji wengi wa kike kuanzia ngazi za chini, na sio kuhitimu na kuweka vyeti ndani tu.
Kozi hiyo, ilianza Jumatatu ambapo washiriki 25 wameshiriki kutoka katika mikoa ya Dar es salaam, Iringa, Ruvuma, Pwani na Tanga na kupewa vyeti na mpira kama kifaa cha kuanzia kazi ya ukocha
Washiriki hao ni Fatuma Omary, Esther Chabruma, Amina Mwinchumu, Sweetie Charles, Pendo John, Berlina Mwaipungu, Mariam Mchaina, Elizabeth Sokoni, Sophia Mkumba, Marry Masatu, Aziza Mbwele, Fadhila Yusuph.
Wengine ni Veneranda Mbano, Mariam Aziz, Hilda Masanche, Chichi Mwidege, Sophia Edward, Asha Rashid, Fatuma Khatibu, Neema Sanga, Hindu Muharami, Tatu Malogo, Komba Alfred, Veronica Ngonyani, Judith Nyatto na Ingridy Kimario.