Wednesday, February 17, 2016

EUROPA LEAGUE: KOCHA WA LIVERPOOL KLOPP ATUA GERMANY NA WACHEZAJI WAKE TAYARI, SPURS NAO WATUA FIORENTINA!

MENEJA wa Liverpool Jurgen Klopp anarudi kwao Germany kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kuiongoza Klabu yake akiwa na Timu yake ambayo Alhamisi Usiku itaingia WWK Arena huko Bavaria kuivaa Augsburg katika Mechi ya Raundi ya Mtoano ya Timu 32 ya UEFA EUROPA LIGI.
Liverpool, ambao hawajafungwa katika Mechi 6 za EUROPA LIGI Msimu huu wakiwa chini ya Klopp tangu ashike hatamu Mwezi Oktoba, wanaingia kwenye Mechi na Augsburg wakitoka kuibonda Aston Villa 6-0 kwenye Mechi ya Ligi Kuu England.
Liverpool inatarajiwa kushusha Kikosi cha nguvu wakiimarishwa na Mastaa wao kadhaa waliokuwa Majeruhi kitambo ambao ni Daniel Sturridge, Philippe Coutinho na Divock Origi ambao walicheza walipoitwanga Villa.

Emre Can
Kwenye Bundesliga, Augsburg wapo Nafasi ya 14 na Jumamosi walitandikwa kwao na Mabingwa Watetezi na Vinara wa Ligi hii ya Germany, Bayern Munich, Bao 3-1.

Huko Stadio Artemio Franchi, Firenze, Italy, Tottenham watacheza na Wenyeji wao Fiorentina kwenye Mechi nyingine ya Raundi ya Mtoano ya Timu 32 ya UEFA EUROPA LIGI.
Msimu uliopita, Fiorentina ndio iliitupa nje Tottenham kwa kuichapa 2-0 Uwanja huu huu lakini nao wakabwagwa na Sevilla ambao ndio walitwaa Taji hilo.


Chini ya Meneja Mauricio Pochettino, Tottenham itawakosa Majeruhi Jan Vertonghen na Clinton N'Jie lakini Nacer Chadli na Nabil Bentaleb huenda wakacheza baada ya maumivu yao kupona. Jumapili iliyopita, Fiorentina, chini ya Kocha Paulo Sousa, waliitwanga Inter Milan 2-1 na kukamata Nafasi ya 3 kwenye Ligi ya Italy Serie A.