Monday, February 29, 2016

KINDA WA MIAKA 18 MARCUS RASHFORD AWASHANGAZA WANASOKA WENGI

NDANI ya Siku 3, Kinda wa Miaka 18, Marcus Rashford, ameibuka na kupiga Bao 4 katika Mechi zake 2 za kwanza kabisa akiichezea Manchester United, na kuibua gumzo kubwa huko England na kila kona ya Dunia.
Majuzi Alhamisi, Marcus Rashford, akichezea Kikosi cha Kwanza cha Man United kwa mara ya kwanza, alipoingizwa bila kutarajiwa kabla ya Mechi kuanza baada ya kuumia Anthony Martial wakati akipasha moto, alipiga Bao 2 wakati Man United inaitwanga FC Midtjylland 5-1 katika Mechi ya UEFA EUROPA LIGI.
Na Jumapili, ndani ya Old Trafford, Marcus Rashford, alipiga Bao 2 tena na kuweka Rekodi ya kuwa Kijana mdogo kabisa katika Historia ya Man United kufunga Bao za Ligi wakati Man United inawabonda Arsenal 3-2 Uwanjani Old Trafford.

Mbali ya Siku hii kuwa ya Marcus Rashford, Wadau wengi sasa wameanza kukata tamaa kwa Arsenal kutwaa Ubingwa Msimu huu hasa baada ya kujikuta sasa wako palepale Nafasi ya 3 wakiwa Pointi 3 nyuma ya Tottenham, walio Nafasi ya Pili, na Pointi 5 nyuma ya Vinara Leicester City. Lakini kilichowaumiza wengi, hasa Wadau wa Arsenal, ni kufungwa na Kikosi dhaifu cha Man United ambacho kilikosa karibu Robo 3 ya Wachezaji wao wa kawaida na kuwatumia Makinda ambao kila Mtu alitegemea watafagiwa na Masupastaa wa Arsenal kina Mesut Ozil, Alexis Sanchez, Aaron Ramsey na kadhalika.

NINI WAMESEMA BAADA YA KIPONDO HIKI:
Arsene Wenger kwa Arsenal:

"Tulitanguliwa kufungwa nah ii ilileta ugumu. Kinachosikitisha tulimiliki sana Mpira na kuruhusu Bao 3. Tumepoteza Pointi 3 muhimu hii Leo na inabidi tushinde Jumatano.”
Alipohojiwa kama kipigo hiki kitaathiri nafasi yao ya kutwaa Ubingwa, Wenger alijibu: “Hakuna anaejua!” Kuhusu Marcus Rashford, Wenger, akikiri kutomjua, alisema: “Alinishangaza kwa mwendo wake golini na akili zake. Huyu ataishangaza Man United!”

Lejendari wa Arsenal Thierry Henry:
"Sidhani hili lingetokea enzi zote wakati nacheza. Huu si uchezaji wa Timu inayosaka Ubingwa. Hili ndio kama shabiki wa Arsenal nalitazama lakini sina hakika Timu hii inaweza kuwa Bingwa. Hakuonyesha! Lakini bado wamo mbio za Ubingwa lakini Leo walikuwa wa pili kwa kila kitu!”
Akimgeukia Rashford, Henry alisema: “Mbali ya kufunga Goli 4 Mechi 2, uchezaji wake na jinsi anavyopenya kwenye nafasi, kumiliki na kuhodhi mpira, kunaonyesha ana dhamira kubwa. Anajua nini kinaendelea, ametulia kwenye Boksi, vile Vichwa na pia anafanya zile kazi ngumu na chafu Uwanjani!”


Louis van Gaal:
"Nasikia fahari kubwa, nimeridhika na nina furaha kwa sababu tulifanya na Shrewsbury, tumefanya na Midtjylland na sasa tumefanya dhidi ya Timu nzuri sana ya Ligi Kuu England, nimefurahishwa!”

Juu ya Marcus Rashford, Van Gaal alisema: “Alicheza vizuri na ile Timu ya Denmark lakini na Arsenal amecheza vizuro mno!”

Marcus Rashford:
"Ilikuwa Gemu yangu ya kwanza kwenye Ligi na ni ajabu. Kupiga Bao 2 ni bonasi!"