Sunday, February 28, 2016

LEO NDANI OLD TRAFFORD, MANCHESTER UNITED v ARSENAL

BAADA ya kufungwa na Sunderland Wiki 2 zilizopita, Manchester United wanasaka ushindi kwenye Ligi Kuu England, BPL, na Leo wako kwao Old Trafford kupambana na Arsenal ambao wako Nafasi ya 3 wakiwania Taji lao la kwanza baada ya Miaka 12.
Ndani ya Old Trafford, Man United wameshinda Mechi 6 na Sare 2 katika Mechi 8 zilizopita dhidi ya Arsenal.
Baada ya kufungwa na Sunderland, Man United sasa wameshinda Mechi 2 mfululizo kwa kuzitoa Shrewsbury Town kwenye Emirates FA Cup na FC Midtjylland kwenye UEFA EUROPA LIGI.
Arsenal wao wameshinda Mechi 2 tu za Ligi katika 6 zilizopita na moja ikiwa ni 2-1 kwa ushindi wa Dakika za mwisho dhidi ya Vinara wa Ligi Leicester City.
Lakini, Juzi wakiwa kwao Emirates, Arsenal walidundwa 2-0 kwenye Mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
WACHEZAJI
David De Gea na Chris Smalling wanaweza kurejea baada ya kupona maumivu yao baada ya wote kuikosa Mechi ya Juzi na FC Midtjylland.
Marcos Rojo na Antonio Valencia nao wamepona lakini Anthony Martial yupo kwenye wasiwasi baada kuumia kabla ya Mechi na Midtjylland kuanza na nafasi yake kuzibwa na Chipukizi Marcus Rashford aliefunga Bao 2.
Majeruhi wengine wa Man United ambao wataikosa Mechi hii ni Matteo Darmian, Marouane Fellaini, Phil Jones, Ashley Young, Wayne Rooney, Will Keane, Bastian Schweinsteiger na Luke Shaw.

Kwa upande wa Arsenal, Gabriel Paulista anategenewa kurudi huku Alex Oxlade-Chamberlain, Tomas Rosicky, Jack Wilshere na Santi Cazorla wakiwa nje kutokana na kuumia.

Kwenye Mechi ya kwanza Msimu huu huko Emirates, Arsenal walishinda 3-0 kwa Bao za ndani ya Dakika 20 za kwanza za Mechi hiyo.