Friday, February 12, 2016

LIGI DARAJA LA KWANZA KUMALIZIKA KESHO, ASHANTI UNITED, AFRICAN LYON NA POLISI TABORA NANI KUUNGANA NA RUVU SHOOTING LIGI KUU?

PAZIA la Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara linafungwa kesho kwa timu za Kundi A na C nazo kupata rasmi timu zao zitakazopanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Tayari timu ya Ruvu Shooting imepanda daraja kupitia Kundi B baada ya kuwa na pointi nyingi mbazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine za kundi hilo.
Katika Kundi A mchuano mkali uko kwa timu tatu, ambazo zote zinaweza kufuzu kwa Ligi Kuu ila itategemea kila timu itachezaje karata zake.
Timu za African Lyon inaoongoza kwa kuwa na pointi 26 na imekaribia kabisa kupanda daraja lakini itategemea na Friend Rangers na Ashanti, ambazo zote zina pointi 23.
African Lyon endapo itafungwa mchezo wake wa leo dhidi ya Ashanti United na Friends Rangers ikaibuka na ushindi dhidi ya Kiluvya, basi Friends watapanda daraja kwa kuwa wana mabao mengi ya kufunga.
Katika Kundi C, timu za Polisi Tabora na Geita Gold ndizo zina nafasi kubwa ya kupenya kufuzu kwa Ligi Kuu Tanzania msimu ujao itategemea na matokeo ya mechi zao za mwisho.

Polisi Tabora wenye pointi 27 leo wanacheza na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora huku Geita Gold yenye pointi 24 wenyewe wanacheza na wachovu JKT Kanembwa ambao tayari wameshashuka daraja.
Hata hivyo, Geita pamoja na kuwa na pointi 24 lakini inasubiri kupewa pointi zake tatu baada ya JKT Oljoro kumpinga maamuzi na kuweka mpira kwapani walipocheza na Geita, iliyokuwa ikiongoza kwa mabao 2-0 wakati mchezo huo unavunjika.
Kwa mujibu wa kanuni na sheria za soka, Geita wanasubiri pointi hizo tatu kwani Oljoro ndio walileta vurugu na kuweka mpira kwani.
Mechi zingine leo ni kati ya Polisi Dar na Polisi Dodoma Uwanja wa Mabatini, Pwani, Mji Mkuu watacheza na Kinondoni Municipal Council FC.
Katika Kundi B Kimondo Super SC watacheza na Kurugenzi (Vwawa), Njombe Mji watacheza na Lipuli FC (Amani), Ruvu Shooting na Polisi Morogoro (Mabatini) na Burkinafaso dhidi ya JKT Mlale (Jamhuri).
Mechi za upande wa Kundi C ni kati ya Mbao FC dhidi ya Polisi Mara (CCM Kirumba).