Thursday, February 11, 2016

LIGI KUU ENGLAND WIKIENDI HII, NANI KUINGIA "TOP 4" NA NANI KUTOKA! REFA ANDRE MARRINER KUSHEZESHA MECHI YA SUNDERLAND v MAN UNITED

WIKIENDI hii huko England ni mitanange inayopambanisha Klabu zilizo Nafasi za 4 za juu kwenye Ligi Kuu England.
Timu zote hizo 4 zinacheza Jumapili kwa Arsenal, ambao wako Nafasi ya 3, kuwakaribisha Vinara Leicester City Uwanjani Emirates huku Leicester wakiwa Pointi 5 mbele ya Arsenal waliofungana Pointi na Tottenham.

Tottenham wao wako Etihad kuivaa Man City ambao wako Nafasi ya 4 wakiwa Pointi 1 nyuma ya Arsenal na Tottenham na Pointi 6 nyuma ya Vinara Leicester.
Huku zikiwa zimebakia Mechi 13 kwa Ligi kumalizika ni wazi Mechi hizi zitatoa fununu kubwa nini mwelekeo wa mbio za Ubingwa na hasa baada ya Leicester City kuinyuka Man City 3-1 huko kwao Etihad katika Mechi iliyopita.
Katika Timu hizi 4, wazoefu wa mbio za Ubingwa ni Arsenal na Man City wakati Tottenham hawajatwaa Ubingwa wa England tangu 1961 na hata kuingia kwao kwenye 4 Bora ya Ligi Kuu England wamewahi mara mbili tu tangu 1992.

Leicester wao ndio wageni kabisa wa mbio hizi na hasa kwa vile kwa Mwongo uliopita walikuwa Madaraja ya chini.

Arsenal, ambao wanasaka Ubingwa wao wa kwanza tangu 2005, wataingia Uwanjani Jumapili wakijiamini hasa baada ya kuinyuka Leicester 5-2 katika Mechi yao ya kwanza ya Ligi Msimu huu huko King Power Stadium matokeo ambayo wengi walitegemea yatawadidimiza Leicester lakini wapi wakaanza mbio za Mechi 10 bila kufungwa kabla kusimamishwa na Liverpool Mwezi Desemba na baada ya hapo wamekwenda Mechi 7 bila kufungwa hadi sasa.

Nao Man City pia watatinga kwao Etihad kucheza na Tottenham huku wakijiamini kutokana na rekodi yao dhidi ya Klabu hiyo ya London baada ya kuinyuka Tottenham Jumla ya Mabao 10 katika Mechi zao 2 zilizopita Uwanjani Etihad huku Sergio Aguero akipiga 6 kati ya hizo.
Pia Mwaka 2014 waliinyuka Tottenham Bao 5-1 huko White Hart Lane lakini Mwezi Septemba katika Mechi yao ya kwanza ya Ligi Msimu huu, Tottenham waliipiga City 4-1.

Mechi hizi za Wikiendi hii zitafunguliwa dimba Jumamosi kwa Mechi ya kwanza kabisa huko Stadium of Light wakati Wenyeji Sunderland watakapocheza na Man United ambao wako Nafasi ya 5 kwenye Ligi wakiwa Pointi 6 nyuma ya Timu ya 4 Man City.
RATIBA KAMILI WIKIENDI HII
Jumamosi 13 Februari 2016
15:45 Sunderland vs Man United

[Mechi  Saa 12:00 Jioni]

Bournemouth vs Stoke
Crystal Palace vs Watford
Everton vs West Brom
Norwich vs West Ham
Swansea vs Southampton
20:30 Chelsea vs Newcastle

Jumapili 14 Februari 2016
15:00 Arsenal vs Leicester
17:05 Aston Villa vs Liverpool 

19:15 Man City vs Tottenham