Thursday, February 11, 2016

MAN UNITED KUVUNJA REKODI YA KLABU ZA UINGEREZA KWA MAPATO!

Manchester United wapo mbioni kuvunja Rekodi ya Uingereza kwa kuwa Klabu ya kwanza kabisa ya kuvuna Mapato ya zaidi ya Pauni Nusu Bilioni kwa Mwaka mmoja licha ya Timu kusuasua Uwanjani.
Sare ya 1-1 ya Jumapili iliyopita huko Stamford Bridge na Chelsea imewaacha wakiwa Nafasi ya 5 kwenye Ligi Kuu England huku wakiwa Pointi 6 nyuma ya Timu ya 4 ambayo ndio Nafasi ya mwisho ya kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao. Pia, Man United sasa wapo kwenye uvumi mkubwa kuwa Meneja wao, Louis van Gaal, atabadilishwa mwishoni mwa Msimu na Jose Mourinho.
Lakini licha ya matatizo hayo, Man United Kibiashara imezidi kuimarika na Leo wametangaza Mapato yao kwa Mwaka yatagonga Pauni Milioni 500 hadi 510 kitu ambacho hakuna Klabu yeyote ya Uingereza imewahi kufikisha.
Mapato kwa Robo ya Pili ya Mwaka yamepanda na kufikia Pauni Milioni 133.8 ikiwa ni ongezeko la Asilimia 26.6 kutoka ya Mwaka uliopita wa Fedha.
Mapato kutokana na Matangazo yamepanda kwa Asilimia 31.3 na yale ya Udhamini kwa Robo ya Pili ya Mwaka yamepanda kwa Pauni Milioni 1.6 na kufikia Pauni Milioni 37.4.