Tuesday, February 16, 2016

MAN UNITED YAMTANGAZA NICKY BUTT MKUU WA CHUO CHA SOKA(ACADEMY)

Manchester United IMEMTEUA Nicky Butt ameteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Soka cha Klabu hiyo.
Butt, mwenye Miaka 41, alikulia Kisoka akiwa Man United na kuichezea Timu Ya Kwanza Mechi 387 kati ya Miaka ya 1992 hadi 2004.
Mwaka 2012 Butt alirejea Klabuni hapo kama Kocha na kuzifundisha Timu za Rizevu na ile ya Vijana wa chini ya Miaka 19, U-19.

Mwenyekiti Mtendaji wa Man United, Ed Woodward, amesema: “Nicky ana urithi na utamaduni wa Klabu kwenye damu yake. Ndie chaguo asilia.”
Uteuzi huu wa Nicky Butt unafuatia mabadiliko kwenye Menejimenti ya Chuo cha Soka baada ya Mkurugenzi wa Chuo hicho, Brian McClair, ambae pia alikuwa Mchezaji wa zamani wa Klabu hiyo, kuondoka Mwezi Juni 2015.
Woodward ameeleza pia ujio wa Butt utaleta ‘msisitizo, nguvu na uzoefu’ kwenye uongozi: “Katika Miaka Minne iliyopita, Wachezaji 15 toka Chuoni wameichezea Timu ya Kwanza, wakicheza Jumla ya Mechi 173 na hii ni rekodi ambayo Klabu inasikia fahari juu yake!”
Akiwa Mchezaji chini ya Sir Alex Ferguson, Nicky Butt alitwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England mara 6, UEFA CHAMPIONS LIGI na kuichezea England mara 39.
Kwenye Msimu wa 2013/14, Nicky Butt aliteuliwa kuwa Msaidizi wa Meneja wa Muda Ryan Giggs, ambae alishika wadhifa huo kwa Mechi 4 za mwisho za Msimu huo baada ya kutimuliwa David Moyes.