Friday, February 12, 2016

RIO FERDINAND ANENA! ASEMA KUMPA KAZI GIGGS NI KUPOTEZA, LABDA JOSE MOURINHO NDIYE WA KUIWEZA MAN UNITED.

Rio Ferdinand anafikiri Manchester United itakuwa inatembea juu ya ganda la ndizi wakimteua Ryan Giggs kama Meneja wao anaefuatia.
Hivi sasa Meneja Louis van Gaal yupo kwenye hatihati kubwa kumaliza Mkataba wake unaoishia Juni 2017 kwa vile Timu inasuasua kupata nafasi ya kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI ikiwa nje ya 4 Bora wakiwa Nafasi ya 5 Pointi 6 nyuma ya Timu ya 4 huku Mechi zikibaki 13.
Hali hii imefanya kuzagaa uvumi kuwa Jose Mourinho, alietimuliwa Chelsea Mwezi Desemba, atamrithi Van Gaal mwishoni mwa Msimu huu ingawa pia Giggs, ambae ni Meneja Msaidizi chini ya Van Gaal, anatajwa pia kuchukua wadhifa huo.
Rio Ferdinand, ambae alicheza pamoja na Giggs kwa Miaka 12 chini ya Sir Alex Ferguson na kutwaa Ligi Kuu England mara 6, anakiri Giggs, ikiwa atakuwa Meneja, ataendeleza utamaduni wa Man United wa kucheza Soka la kuvutia na kuwatumia Chipukizi kama desturi ya Klabu lakini itakuwa ni Kamari kumteua yeye. Rio, ambae sasa ni Mchambuzi wa Soka baada kustaafu, ameeleza: “Jina la Jose Mourinho linatajwa. Kama unahitaji Mtu mwenye wasifu wa ushindi Ligi Kuu na Nchi nyingine basi ni yeye. Lakini ukitaka Mtu anaejua falsafa, anaeheshimu falsafa, anaetambulika kwa Mashabiki, anaeijua Klabu nje ndani, ingawa ni bahati nasibu, basi ni Ryan Giggs!”

Ferdinand, ambae aliichezea Man United Mechi 455, ameongeza: “Tangu niondoke, nilijua hali itakuwa ngumu. Lakini nilitegemea zaidi. Nadhani tatizo ni staili ya uchezaji.”