Tuesday, February 16, 2016

SIR BOBBY CHARTON ATUZWA OLD TRAFFORD!

Jukwaa la Kusini la Uwanjani Old Trafford ambalo ndio sehemu pekee ya Uwanja wa awali uliojengwa Mwaka 1910 ambayo imebakia litabatizwa Jina la Lejendari wa Manchester United na kuitwa Jukwaa la Sir Bobby Charlton.
Sir Bobby Charlton, ambae sasa ni Mkurugenzi wa Klabu hiyo, alikuwa Mchezaji mahiri wa Man United na ambae mpaka sasa ndie anashikilia Rekodi ya Ufungaji Bora katika Historia ya Man United akiwa na Mabao 249.
Jina hilo jipya litaanuliwa rasmi hapo Tarehe 2 Aprili 2016 mbele ya Watazamaji 75,000 wakati wa Mechi ya Man United na Everton ambapo pia watakuwepo Watu muhimu katika maisha ya Lejendari huyo.
Sir Bobby Charlton alijiunga na Man United kama Mchezaji Mwanafunzi Mwaka 1953 na kuanza kucheza Mechi yake ya kwanza kabisa Oktoba 1956 ambapo alicheza Jumla ya Mechi 758 hadi anastaafu.

Mbali ya kuishikilia Rekodi ya Klabu ya Bao nyingi ambayo sasa inakimbizwa na Kepteni Wayne Rooney aliebakiza Bao 6 kuikamata, Sir Bobby pia alishikilia Rekodi ya kuwa Mfungaji Bora wa Timu ya Taifa ya England hadi Septemba 2015 alipokuwa na Bao 49 kwa Mechi 106 na Wayne Rooney kuivunja kwa kufunga Bao 50.Sir Bobby Charlton Enzi hizo kwenye kabumbu