Friday, February 26, 2016

UCHAGUZI WA URAIS WA FIFA WAENDELEA..MJINI ZURICH WAINGIA RAUNDI YA PILI, GIANNI INFANTINO ATAMBA


Upigaji kura wa kuamua atakayekuwa rais wa shirikisho la soka duniani Fifa umeingia raundi ya pili baada ya kukosekana kwa mshindi wa moja kwa moja raundi ya kwanza.

Mshindi alitakiwa kupata theluthi mbili ya kura.

Katibu mkuu wa Uefa Gianni Infantino ndiye aliyepata kura nyingi akiwa na kura 88, akiwa na kura tatu zaidi ya mpinzani wake wa karibu Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa.

Prince Ali bin al-Hussein alifuata akiwa na kura 27, huku Jerome Champagne akiwa wa mwisho na kula saba. Mfanyabiashara wa Afrika Kusini Tokyo Sexwale alijiondoa kabla ya upigaji kura kuanza.
Matokeo ya raundi ya kwanza
Prince Ali - 27
Sheikh Salman - 85
Jerome Champagne - 7
Gianni Infantino - 88

Kwenye raundi ya pili, wagombea wote watapigiwa kura na iwapo kuna atakayepata zaidi ya nusu ya kura, atatangazwa mshindi.

Akikosekana mtu kama huyo, basi uchaguzi utaingia raundi ya tatu na mgombea aliyepata kura chache zaidi raundi ya kwanza ataondolewa.
Wajumbe kutoka mataifa 207 yanayotambuliwa na Fifa duniani wanashiriki uchaguzi huo mjini Zurich kuamua mrithi wa Sepp Blatter.
Kabla ya upigaji kura kuanza, mageuzi kadha yalipitishwa, lengo likiwa kufanya Fifa kuwa na uwazi na uwajibikaji zaidi.
Kufuatia mabadiliko hayo, mishahara yote ya maafisa wa Fifa inafaa kuwekwa wazi siku za usoni.
Kutakuwa pia na kipimo kwenye muhula wa urais.
Baraza jipya pia litaundwa kuchukua nafasi ya kamati kuu tendaji, ambalo litakuwa na mwakilishi mwanamke kutoka kila shirikisho.