Tuesday, February 9, 2016

WAYNE ROONEY AMLINDA MEMPHIS DEPAY, ATAKA WAFUNGE MIDOMO YAO WANAOMSAKAMA KWA BAO LA KUSAWAZISHA CHELSEA!

NAHODHA wa  Manchester United Wayne Rooney amesema Memphis Depay asilaumiwe kwa Bao la Dakika za Majeruhi ambalo liliwaokoa Chelsea na kuwapa Sare ya 1-1 Uwanjani kwao Stamford Bridge kwenye Mechi ya Ligi Kuu England.
Huko England, kuliibuka wimbi kubwa la kumlaumu Memphis kwa Pasi yake mbovu kwa Morgan Schneiderlin iliyotoa mwanya kwa Shambulizi la Chelsea katika Dakika za Majeruhi na kuzaa Bao la Diego Costa alipoifungia Chelsea Bao la kusawazisha.
Memphis, ambae ametimiza Miaka 22 Wiki hii, hajaanza Mechi yeyote ya Man United tangu Siku ya Boksing Dei ambapo Pasi yake mbovu kwa Kipa David de Gea ndio iliyozaa Bao la kwanza kwa Stoke City huko Britannia Stadium walipofungwa 2-0 na Stoke.

Licha ya Memphis kutocheza kiwango katika Miezi yake 6 ya mwanzo akiwa na Man United tangu ahamie hapo kutoka PSV Eindhoven kwa Dau la Pauni Milioni 25, Kepteni Rooney ametetea: “Wote tunahuzunika. Memphis ni Mchezaji mzuri mno na hilo hutokea, sote tunatoa Pasi mbovu. Vitu vingi hutokea tangu pale ukitoa Pasi mbovu na wanapofunga hivyo si sahihi kumlaumu Memphis. Kuna vitu vingine vilitokea na ndio maana wakafunga.”
Katika Mechi hiyo ya Stamford Bridge hapo Jumapili, Jesse Lingard aliipa Man United Bao katika Dakika ya 61 na Rooney amekiri walikosea kuruhusu presha toka kwa Chelsea baada ya Bao lao.
Alisema: “Gemu ilivurugika na tulitoa frikiki nyingi na tulishindwa kupanda mbele. Lakini ukicheza na Chelsea, wakati mwingine ni ngumu, kwa sababu wanakusukumeni nyuma na hawachezi kwa Mfumo unaotambulika na hivyo ni ngumu kujua utajihami vipi!”