Sunday, March 27, 2016

AFCON 2017 – KUNDI LA TANZANIA: CHAD YAJITOA KWA UKATA WA FEDHA, YAVURUGA KUNDI G!

CHAD, ambayo Majuzi ililtandikwa Bao 1-0 na Tanzania wakiwa kwao huko Mjini N’Djamena, Leo wametangaza kujitoa Mashindano haya ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2017, na kulivuruga Kundi G ambalo pia wapo Nigeria na Egypt.
Kujitoa kwa Chad, ambao Kesho Jumatatu Machi 28 walipaswa kushuka Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kurudiana na Tanzania, kulitangazwa hii Leo na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Chad, Moctar Mahamoud, ambae alisema hawana Fedha na hivyo wameshindwa kuisafirisha Timu kwenda Dar es Salaam.

Kujitoa kwa Chad kumeacha Kundi G liwe na Mechi moja tu Wiki huu hapo Jumanne huko Borg El Arab Stadium Mjini Alexandria wakati Egypt ikicheza tena na Nigeria baada ya Juzi kutoka Sare 1-1 huko Kaduna.

Kwa mujibu wa Kanuni za CAF, Mechi za Chad za Kundi G sasa zinafutwa na kuiacha Egypt ikiwa kileleni ikiwa na Pointi 4, ikifuata Nigeria Pointi 2 na Tanzania Pointi 1.