Tuesday, March 29, 2016

ARSENE WENGER ASEMA BADO YUPO GUNNERS KWA MSIMU UJAO..LICHA YA KUSAKAMWA NA MASHABIKI

HUKU akisongwa na presha kubwa ya kumaliza Msimu mwingine bila Taji la England na bila Kombe lolote, Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesisitiza bado atakuwepo Emirates licha ya kusakamwa atimue.
Baada ya kutupwa nje ya FA CUP, Kombe ambalo walilitwaa kwa Misimu Miwili mfululizo iliyopita, na pia kutolewa toka UEFA CHAMPIONS LIGI huku wakisuasua kwenye Ligi Kuu England wakiwa Nafasi ya 3 na Pointi 11 nyuma ya Vinara Leicester City, Wenger amekuwa akishambuliwa toka kila upande.
Lakini Wenger, ambae Msimu ujao ndio Mwaka wake wa mwisho wa Mkataba wake wa sasa wa Miaka Mitatu, amesisitiza atarejea akiwa tayari kupigana tena akiiongoza Arsenal.

Ameeleza: “Hatukustahili kupondwa. Mimi natoa nguvu zangu zote kwa Klabu ninayoipenda na kama Mashabiki watachangia mapenzi hayo ni bora. Nina ari na nina hakika nitakuwepo Msimu ujao!”

Wikiendi hii inayokuja, Arsenal wako kwao Emirates kucheza na Watford Timu ambayo ndio ilwang’oa toka FA CUP hapo hapo Emirates Wiki 2 zilizopita kwa kuwafunga 2-1.