Thursday, March 31, 2016

GARY NEVILLE ATIMULIWA VALENCIA!

BEKI wa zamani wa Manchester United na England Gary Neville ametimuliwa toka Klabu ya Spain Valencia ambako alidumu kama Kocha Mkuu kwa muda usiozidi Miezi Minne.
Neville, mwenye Miaka 41 na ambae pia ni Msaidizi wa Meneja wa Timu ya Taifa ya England Roy Hodgson, aliteuliwa kuiongoza Valencia Mwezi Desemba.
Tangu wakati huo, Valencia ilishinda Mechi 3 tu kati ya 16 za La Liga na Mechi 10 kati ya 28 walizocheza chini ya Neville.
Huku akikiri kuwa alitaka abaki Valencia na pia kuungama kuwa matokeo hayakuwa ya kiwango chake au Klabu, Neville amekubali amepaswa kuwajibika.
Balaa na kusakamwa kwa Neville kutakiwa kung’oka na Mashabiki wa Valencia kulianza Mwezi Februari waliponyukwa Bao 7-0 na Barcelona kwenye Mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Copa del Rey.
Mbali ya kutamkwa kutimuliwa kwa Gary Neville lakini hatima ya Mdogo wake Phil Neville ambae ni mmoja wa Makocha wa Valencia na alikuwa hapo hata kabla Gary kutua huko bado hakujawekwa bayana.
Kwa sasa Valencia itakuwa chini ya Meneja Msaidizi wa zamani wa Liverpool Pako Ayestaran, mwenye Miaka 53, hadi mwishoni mwa Msimu.
Kwenye La Liga, Valencia wapo Nafasi ya 14 wakiwa Pointi 6 tu juu ya zile Timu za kushushwa Daraja huku Gemu zikibaki 8 hadi Msimu kwisha.