Friday, March 11, 2016

KIPIGO CHA BAO 2-0 ANFIELD, SCHOLES AWASHAMBULIA WACHEZAJI NA VAN GAAL

LEJENDARI wa Manchester United, Paul Scholes, amefyatua maneno makali mno kwa Wachezaji wa Timu hiyo na Meneja wao Louis van Gaal kufuatia kipigo chao cha 2-0 huko Anfield Alhamisi Usiku katika Mechi ta Kwanza ya Raundi ya Mtoano ya Timu 16 ya EUROPA LIGI.
Scholes, akiwa pamoja na Mchezaji mwingine wa zamani wa Man United Rio Ferdinand kwenye uchambuzu wa Mechi hiyo katika Kituo cha TV cha BT Sport, alisema: “Man United walikuwa ni aibu!”

 Aliongeza: “Ukiwa 2-0 nyuma bado upo kwenye Gemu, na ukiwa Man United kuna viwango vinavyopaswa kubakia. Sisi tulipochipukia kama Wachezaji walikuwepo Wachezaji wa mifano kama Bryan Robson, Roy Keane, Paul Ince na Steve Bruce wakiweka viwango na ilibidi sisi tufikie viwango hivyo, sasa hamna!”
Scholes alicharuka: “Mimi na Rio, wakati tukicheza, tuliweka viwango kwa Wachezaji wengine, Meneja Sir Alex, aliweka viwango kwa David Moyes, kwa Louis van Gaal, na hakuna Mtu aliefikia! Leo Liverpool walikuwa wanajua nini wanakicheza na Man United walibaki mbumbumbu tu!”
Rio Ferdinand alimuunga mkono Scholes kwa kusema: “Kutoonekana upiganaji, kukosa hima kwenye Timu na kutoelewana Kitimu ni kosa na inabidi wabadilike mno kwa Mechi ya marudio huko Old Trafford”
Rio aliongeza: “Kukaa hapa Anfield, miongoni mwa Mashabiki wa Liverpool, si kitu rahisi. Hamna visingizio, unamtazama Meneja lakini Wachezaji Uwanjani wanapaswa wajiulize, lazima wacheze. Na Leo hatukuona, inasikitisha, hamna kuelewana na mfumo hamna!”