Tuesday, March 29, 2016

LIVERPOOL WAONGEZA NIA KUMSAINI MARIO GOTZE

Liverpool wana nia ya kumsaini Mchezaji wa Bayern Munich Mario Gotze kwa mujibu wa vyanzo toka huko England.
Gotze, Kiungo wa Miaka 23, anahusishwa na kujiunga na Liverpool hasa kwa vile Meneja wa sasa wa Klabu hiyo, Jurgen Klopp, alikuwa pamoja na Mchezaji huyo walipokuwa wote Klabu ya Borussia Dortmund huko Germany.

Gotze, ambae ndie alifunga Bao pekee na la ushindi kwenye Fainali ya Kombe la Dunia huko Brazil Mwaka 2014 Germany ilipoifunga Argentina 1-0, amekuwa hana namba huko Bayern chini ya Kocha Pep Guardiola na hajaanza Mechi tangu Oktoba.
Guardiola sasa atajiunga na Manchester City mwishoni mwa Msimu na Bayern kuwa chini ya Carlo Ancelotti huku hatima ya Gotze ikiwa njia panda na akiwa amebakisha Mwaka mmoja tu kwenye Mkataba wake na Bayern.

Mchezaji huyo aling’ara mno alipokuwa na Klopp huko Dortmund tangu Meneja huyo ampe namba kwa mara ya kwanza Mwaka 2010 alipokuwa na Miaka 18 tu.
Chini ya Klopp, Gotze aliichezea Dortmund Mechi 99 na kufunga Bao 22 kabla kuhamia Bayern Mwaka 2013 kwa Dau la Pauni Milioni 31.5.

Inaaminika Liverpool wanaamini wanaweza kumsaini Gotze kwa Dau la Pauni Milioni 20 hasa ukizingatia muda wa Mkataba wake na Bayern uliobakia.