Monday, March 14, 2016

PSG YATWAA TAJI LIGUE 1 KIREKODI, IBRAHIMOVIC APIGA 4 IKIUA 9-0!

VIGOGO wa Ufaransa Paris Saint-Germain, wakiongozwa na Bao 4 za Supastaa Zlatan Ibrahimovic, Jana waliitwanga Troyes 9-0 na kutwaa Taji la Ubingwa wa Ligi 1 France kwa mara ya 4 mfululizo huku wakiwa na Mechi 9 mkononi.
Ushindi huu umekuja Siku 4 tu baada ya kuitupa nje Chelsea kutoka UEFA CHAMPIONS LIGI baada ya kuinyuka 2-1 huko Stamford Bridge na kuingia Robo Fainali.

Kwa kutwaa Taji hilo la France, PSG, chini ya Kocha Laurent Blanc, wameifuta Rekodi ya Lyon waliotwaa Ubingwa Mwaka 2007, chini ya Gerard Houllier, huku wakiwa na Mechi 5 mkononi.
Wakicheza Ugenini hapo Jana huko Stade de l'Aube, Bao 3 ndani ya Dakika 6 za Kipindi cha Kwanza zilizofungwa na Edinson Cavani, Pastore na Adrien Rabiot ziliwatuliza Mabingwa hao.
Kisha akaja Ibrahimovic na kupiga Bao la 3 katika Dakika 10 za Kipindi cha Pili na kuifanya PSG iongoze 6-0.

Bao za 7, 8 na 9 zilifungwa na Matthieu Saunier, aliejifunga mwenyewe, Edinson Cavani na Ibrahimovic.