Friday, March 4, 2016

RATIBA LIGI KUU ENGLAND WIKIENDI HII, MAPEMA JUMAMOSI NI DABI YA NGUVU SPURS v ARSENAL

BAADA ya Timu zote kutandikwa Jumatano Usiku, Tottenham Hotspur na Arsenal wana nafasi kubwa kurejea kwenye reli za mbio za Ubingwa wa Ligi Kuu England hapo Jumamosi wakikutana huko White Hart Lane katika Dabi ya London ya Kaskazini.
Siku zote Mechi kati ya Timu hizi ni za ushindani mkubwa sana lakini safari hii zote, wakiwa Nafasi ya Pili na ya Tatu, zipo kwenye mbio za Ubingwa zikiwafukuza Vinara wa Ligi Leicester City.
Jumatano Spurs walimaliza mbio zao za kushinda Mechi 6 mfululizo kwa kufungwa 1-0 huko Upton Park wakati Arsenal wakipokea kichapo cha 2-1 kwao Emirates mikononi mwa Swansea City kikiwa ni kipigo cha pili mfululizo kwenye Ligi baada ya Jumapili iliyopita kutandikwa 3-2 na Man United huko Old Trafford.
Leicester, ambao walitoka Sare 2-2 na West Bromwich Albion hapo Jumanne, wanaongoza Ligi wakiwa na Pointi 57 na Spurs wako Nafasi ya Pili wakiwa na Pointi 54, Arsenal wapo wa 3 wakiwa na Pointi 51 wakifuata Man City walio Nafasi ya 4 wakiwa na Pointi 47 na Mechi 1 mkononi.

Man City, ambao Jumatano walinyukwa 3-0 na Liverpool huko Anfield, wana Pointi sawa na Timu ya 5 Man United ambao waliifunga Watford 1-0.
Hii ni mara ya kwanza kwa Spurs kuwa juu kwenye Msimamo wa Ligi tangu 1985 na hii inaleta changamoto kubwa kwenye Dabi hii na Arsenal.

Wakati Spurs ikiimarika kwa kurudi Kikosini kwa Wachezaji wao walikuwa kwenye maumivu kama vile Mousa Dembele na Dele Alli, Arsenal wamepata pigo baada ya Mechi yao ya Jumatano kufuatia kuumia Kipa wao Petr Cech na Sentahafu Laurent Koscielny na wote wataikosa Dabi hii.
Arsenal pia wanatinga kwenye Dabi hii wakiwa hawajashinda katika Mechi 4 ikiwa ni pamoja na kufungwa Mechi 3 mfululizo kwa mara ya kwanza tangu 2010.
Katika mlolongo huo, Arsenal walitoka 0-0 na Hull City kwenye FA CUP, kuchapwa 2-0 na Barcelona kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI, na kwenye Ligi Kuu England kupigwa 3-2 na Man United na kufungwa 2-1 na Swansea.
Hali hiyo imemtia kiwewe Meneja wao Arsene Wenger kiasi cha kuungama hadharani huku akitaka Kikosi chake kirudie hali yao ya msingi na kugangamala.
Kwenye Mechi nyingine za Wikiendi hii, Leicester watakuwa Ugenini kucheza na Watford wakati City wapo kwao Etihad kucheza na Timu ya mkiani Aston Villa.
Manchester United wapo Ugenini huko The Hawthorns kucheza na West Brom Siku ya Jumapili wakati Mabingwa Watetezi Chelsea wako Nyumbani Stamford Bridge kucheza na Stoke City hapo Jumamosi.
LIGI KUU ENGLANDRATIBA
Jumamosi Machi 5

15:45 Tottenham v Arsenal
[Mechi zote Saa 18:00]
Southampton v Sunderland
Man City v Aston Villa
Chelsea v Stoke City
Everton v West Ham
Swansea City v Norwich City
Newcastle v Bournemouth
Watford v Leicester City

Jumapili Machi 6
16:30 Crystal Palace v Liverpool
19:00 West Brom v Man United