Thursday, March 31, 2016

SIR ALEX FERGUSON ASEMA LEICESTER CITY WANASTAHILI KUTWAA UBINGWA MSIMU HUU!

Sir Alex Ferguson amesema Leicester City wanastahili kutwaa Ubingwa wa BPL, Ligi Kuu England.
Leicester, ambao wengi walidhani watakuwa wakipigania kutoshushwa Daraja Msimu huu, sasa wanaongoza BPL wakiwa Pointi 5 mbele huku Mechi zimebaki 7.
Kwa wengi, Leicester, chini ya Meneja kutoka Italy Claudio Ranieri, kutwaa Ubingwa itakuwa ni muujiza usiotarajiwa.
Lakini Sir Alex Ferguson anaamini Leicester hawatatetereka na watafikia tamati wakiwa Mabingwa.
Akiongea na Sky Sports, Meneja huyo Lejendari wa Manchester United amesema: “Leicester wana ari na wameonyesha wao ni Timu bora bila kuyumba Msimu mzima na wanastahili kushinda.”

“Ulitegemea kutokuwa na uzoefu kungeweza kuwagharimu lakini wao wana nguvu na umoja na hilo linaonyesha litawafikisha mwisho wakiwa Washindi. Kwa mfano wameshinda Mechi zao kadhaa za mwisho kwa 1-0. Niliwahi kuwa na Msimu na Man United na tulishinda 1-0 Mechi 8 na hilo lilitupa Ubingwa. Ushindi wa 1-0 ni muhimu kwa sababu inaonyesha wana umoja, hawafungwi!’
Ferguson aliongeza: “Wana ari kubwa na hawana mchecheto na hali waliyoko hivi sasa na hilo ni muhimu. Sioni kama wana mchecheto na hiyo ni sababu ya Meneja wao ambae anawatuliza. Ni jambo zuri sana, wanaleta upepo mpya na hii ni safi sana kwa Gemu!”
Sir Alex Ferguson, ambae alitwaa Ubingwa mara 13 akiwa na Man United, anaamini tishio pekee kwa Leicester ni kutoka kwa Tottenham tu.

Spurs, ambao wako Nafasi ya Pili wakiwa Pointi 5 nyuma ya Leicester, Jumamosi wanasafiri kwenda Anfield kucheza na Liverpoon.
Ferguson ameeleza: “Nawaona Tottenham pekee ndio hatari kwa Leicester. Tottenham, kwa sasa, wanatandaza Soka safi kupita Kikosi chochote chao katika Miaka ya hivi karibuni. Lakini Leicester wako mbele. Nadhani watafika mwisho.”