Monday, March 21, 2016

STARS YAJIFUA D'JAMENA LEO..KUIVAA CHAD JUMATANO!

RAIS ZFA KUIONGOZA STARS CHAD        Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ravia Idarus Faina ndiye mkuu wa msafara wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, anatarajiwa kuondoka Dar es salaam kesho Jumanne alfajiri pamoja na wachezaji wengine kuelekea nchini Chad kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2017.
Kundi hilo la pili lenye wachezaji 8, linatarajiwa kuungana na mshambuliaji wa klabu ya TP Mazembe Thomas Ulimwengu kesho Jumanne asubuhi Addis Ababa kisha kuunganisha safari ya kuelekea nchini Chad wanapotarajiwa kufika saa 6 mchana.
Wachezaji wanaotarajiwa kusafiri kesho Jumanne alfajiri kuelekea Chad kwa shirika la ndege la Ethiopia ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika, Himid Mao, Farid Mussa na John Bocco.
Kesho Jumanne wachezaji wote watafanya mazoezi mepesi ya mwisho ya pamoja katika uwanja wa Omnisport Idriss Mahamat Ouya saa 9 mchana, kabla ya kuwavaa wenyeji siku ya Jumatano katika uwanja huo huo. 


STARS YAJIFUA D'JAMENA
Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager leo imefanya mazoezi katika uwanja wa Omnisports Idriss Mahamat Ouya ulipo katika jiji la D’jamena ikiwa ni maandalizi ya mchezo dhidi ya wenyeji Chad siku ya Jumatano.
Taifa Stars imefanya mazoezi kuanzia majira ya saa 9 alasiri, ikiwa ni sawa na muda utakaochezwa mchezo siku ya Jumatano sawa na saa 11 kwa saa za nyumbani Tanzania na Afrika Mashariki.
Akiongelea maandalizi ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Taif Stars Charles Boniface Mkwasa amesema anashukuru vijana wake waliotangulia wamefika salama, hakuna majeruhi na wote wameweza kufanya mazoezi aliyoyapangilia.
“Hapa D’jamena hali ya hewa ni joto kali tofauti na nyumbani, kwa hizi siku mbili tutakazofanya mazoezi hapa, naimani vijana wataweza kuzoea hali ya hewa na kufanya vizuri katika mchezo wa Jumatano” alisema Mkwasa.
Mkwasa amesema wachezaji wake wametoka katika vilabu vyao ambavyo vilikua na michezo mwishoni mwa wiki, wote bado wako fit kikubwa wanafanya maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mchezo huo.
“Hatujapata muda mrefu wa kufanya mazoezi kwa pamoja, wachezaji walikua na majukumu katika vilabu vyao, nashukuru wote wamewasili wakiwa salama na kesho wataungana na wachezaji wenzao wanaokuja katika kundi la pili kwa ajili ya mazoezi ya mwisho na mchezo wenyewe” aliongeza Mkwasa.