Friday, March 4, 2016

TWIGA STARS UGONJWA, YAKUBALI KICHAPO NYUMBANI CHA BAO 2-1 KUTOKA KWA ZIMBABWE JIONI HII

TIMU ya soka ya Taifa ya soka ya wanawake ‘Twiga Stars’ leo imejikuta katika wakati mgumu baada ya kufungwa mabao 2-1 na Zimbabwe ‘Mighty Warriors’ katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika.
Mchezo huo ulifanyika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam, ambapo sasa Twiga Stars ili isonge mbele italazimika kushinda mabao zitakaporudiana nchini Zimbabwe wiki mbili zijazo.


Zimbabwe, wanayotoka wachezaji nyota wa Yanga, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma, pamoja na kiungo wa Simba, Justice Majabvi, walionesha umahiri mkubwa na kuonekana kana kwamba wao ndiyo wenyeji.
Twiga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17, mfungaji akiwa Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, kabla ya Zimbabwe kusawazisha dakika ya 20, mfungaji Daisy Kaitano.
Dakika ya 46, Zimbabwe ilipata bao la pili mfungaji akiwa Erina Jeke akiunganisha krosi ya Eunice Chibanda.
Twiga Stars licha ya kupoteza mchezo huo ilijitahidi kucheza kwa nguvu, lakini umaliziaji haukua mzuri.
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Nasra Juma itabidi afanye kazi ya ziada kuwanoa vijana wake kuhakikisha nao wanaenda kushinda katika mchezo wa marudiano.
Mechi ya marudiano itachezwa Zimbabwe Machi 18 ambapo timu itakayovuka raundi hiyo itamenyana na mshindi kati ya Zambia na Namibia. Fainali za michuano hiyo zimepangwa kufanyika Cameroon baadaye mwaka huu.