Monday, March 21, 2016

WACHAMBUZI WAMSIFIA VAN GAAL KWA KUTUMIA CHIPUKIZI!


Louis van Gaal anastahili sifa kwa kuwaamini Wachezaji Chipukizi wa Manchester United na kuwapanga katika Mechi kubwa kwa mujibu wa Mchambuzi wa Sky Sports ya Uingereza, Graeme Souness.
Marcus Rashford, mwenye Miaka 18, Jana alifunga Bao la ushindi Uwanjani Etihad wakati Man United inaitungua 1-0 Man City katika Mechi ya BPL, Ligi Kuu Englnd.
Chipukizi wengine waliocheza Dabi hiyo ya Jiji la Manchester na kung’ara ni Jesse Lingard na Anthony Martial.
Kabla ya Mechi hiyo, Souness, ambae ni Mchezaji na Meneja wa zamani wa Liverpool, alimponda Van Gaal kwa kupanga ‘Watoto Wadogo’ katika Mechi kubwa lakini baadae akaungama kwa kusema: “Nadhani Man United watapata moyo zaidi kwa jinsi Chipukizi wao walivyocheza hasa Kipindi cha Kwanza. Nadhani Martial atakuwa nyota mkubwa hasa ukizingatia ana Miaka 20 tu. United walikuwa wazuri na Meneja wao anastahili pongezi. Tunamshambulia kila wakati lakini anastahili sifa.”
Aliongeza: “Ukifikiria De Gea aliokoa Mipira Mitatu tu katika Dakika 90, hilo linakwambia Wachezaji wa mbele walifanya kazi nzuri sana!”

Mchambuzi mwingine wa Sky Sports, Niall Quinn, alieichezea Sunderland, pia alikoshwa na Chipukizi wa Man United na kukiri kuna wakati kwenye Mechi hiyo Man United walionekana kama ile Timu yao ya zamani iliyotisha.