Friday, April 22, 2016

HATIMAYE MENEJA WA LEICESTER AFUNGUKIA UBINGWA! ASEMA WANAPIGANIA UBINGWA KWA SASA!

MENEJA wa Leicester City Claudio Ranieri anaamini ni ‘sasa au hamna’ ikiwa watataka kutwaa Ubingwa wa BPL, Ligi Kuu England, Msimu huu ambao wanaongoza wakiwa Pointi 5 mbele huku Mechi zimebaki 4 tu.
Tayari Leicester wamefanikiwa kufuzu kucheza UCL, UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao lakini mkazo wa sasa wa Ranieri ni kutwaa Ubingwa.
Ranieri ametamka: “Ni Mwaka huu au hamna tena. Tumefanikiwa kuingia UCL na ni mafanikio makubwa mno lakini sasa tunataka kutwaa Ubingwa kwa nguvu zetu zote, mioyo yetu yote, roho zote, na kila kitu!”
Ranieri ameongeza: “Tunahitaji Pointi 8 na ni Mabingwa na tutajaribu hilo!”

Mafanikio ya Leicester Msimu huu na uwezo wao kutwaa Ubingwa wa England mbele ya Vigogo wa kawaida wa England kunafananishwa na ile Timu iliyoongozwa na Meneja Lejendari, Brian Clough, Nottingham Forest ya Miaka ya 1970 na mapema 1980.
Forest ilitwaa Ubingwa wa Daraja la Kwanza la England [Kabla Ligi Kuu kuanzishwa] Mwaka 1978 ukiwa ni Msimu wao wa kwanza tu humo tangu wapande Daraja na pia Msimu huo huo kutwaa Makombe ya Ulaya.
Wengi huko England wanadai walichokifanya Leicester Msimu huu ni miujiza lakini Ranieri amesema: “Si miujiza. Ni kitu cha ajabu. Ni kitu spesho na ndio maana nasema ‘Ni sasa au hamna’ kwa sababu Msimu ujao utakuwa tofauti. Vigogo watajiimarisha na kuwa imara zaidi!”
Mbali ya kufanya kazi ya Umeneja England ambako pia alikuwa na Chelsea, Ranieri pia alifundisha huko kwao Italy, Spain na France lakini hajawahi kutwaa Ubingwa.
Lakini Ranieri, mwenye Miaka 64, binafsi hajali kuhusu kutwaa Ubingwa na kueleza: “Nafurahi nikiona Watu wamefurahi. Soka ni shoo. Naamini tukishinda Mechi Watu hurudi makwao kwa Familia zao na furaha. Wanaenda kazini na furaha – hilo ni zuri kwangu!”

Aliongeza: “Tangu mwanzo Mashabiki walikuja kwangu na mioyo yao na kuanza kuimba nyimbo na mimi. Hilo zuri. Najua wengine walihoji kwanini Ranieri? Lakini Mashabiki wako nyuma yangu. Wana furaha!”

Jumapili Leicester wapo Nyumbani King Power Stadium kucheza na Swansea bila ya Shujaa wao mkubwa Straika Jamie Vardy, aliewafungia Bao 22 Msimu huu, kwa vile yuko Kifungoni lakini Ranieri hana shaka.
Amesema: “Bila ya yeye sina Vardy mwingine lakini bila yake tunaweza kufanya kitu spesho!”

MECHI ZA LEICESTER CITY ZILIZOBAKI
Jumapili Aprili 24

18:15 Leicester v Swansea
Jumapili Mei 1
16:05 Man Utd v Leicester

Jumamosi Mei 7
19:30 Leicester v Everton
Jumapili Mei 15
17:00 Chelsea v Leicester