Tuesday, April 12, 2016

KOMBE LA SHIRIKISHO: SIMBA YABUTULIWA NJE, DROO NUSU FAINALI NI YANGA, AZAM, MWADUI NA COASTAL! DROO KUFANYIKA "LIVE" AZAM TV LEO JUMANNE USIKU SAA 3!

ROBO FAINALI ya mwisho ya Kombe la Shirikisho, kiudhamini linaitwa Azam Sports Federation Cup, imefanyika Leo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam na Coastal Union kuitoa Simba kwa Bao 2-1.
Coastal sasa wanajumuika na Yanga, Azam FC na Mwadui kwenye Droo ya kupanga Mechi za Nusu Fainali za Kombe hili itakayofanyika Jumanne Aprili 12 Saa 3 Usiku na kurushwa moja kwa moja na Kituo cha TV cha Azam Two.

Hii Leo huko Uwanja wa Taifa Simba ilishusha Kikosi kizito lakini ikajikuta ikitanguliwa
Kwa Bao 1 Dakika ya 19 kwa Frikiki ya Mita 20 ya Youssouf Sabo, Mchezaji wa Cameroun aliewahi kufanya Majaribio Yanga.

Simba walisawazisha Bao hilo katika Dakika ya 47 kupitia Straika wao wa Uganda Hamisi Kiiza alieingizwa Kipindi cha Pili lakini Coastal, ambao wako mkiani mwa Ligi Kuu Vodacom na safari yao kucheza Daraja la chini imewaiva, walichomeka Bao la ushindi Dakika ya 85 kwa Penati iliyopigwa na Youssouf Sabo.

Mshindi wa hili Kombe la Shirikisho ataiwakilisha Tanzania mwaka 2017 katika Mashindano ya CAF ya Kombe la Shirikisho.