Wednesday, April 20, 2016

MASHABIKI WA ARSENAL WAMTAKA ARSENE WENGER ANG’OKE! WACHACHE ‘WAISUSA’ MECHI YAO NA WEST BROM ALBION UWANJANI EMIRATES!

Arsene Wenger amesema atabakia Arsenal licha ya kundi kubwa la Mashabiki kumtaka ang’oke mwishoni mwa Msimu huu.
Mfaransa huyo amesema hajali kuhusu kundi kubwa la Washabiki wa Klabu hiyo wenye Tiketi za Msimu mzima kuhudhuria Mechi za Nyumbani za Uwanjani Emirates kuzimwaga Tiketi zao na kuruhusu nafasi zao ziuzwe upya.
Kama ilivyo Misimu iliyopita, Msimu huu Arsenal walianza vyema lakini tangu 2016 ianze Timu hiyo imedumaa na sasa imetupwa nje ya kinyang’anyiro cha Ubingwa na wamebakiwa na vita kubwa ya kuwemo kwenye 4 Bora za Ligi Kuu England.
Ripoti za Magazeti kadhaa ya Uingereza zimedai Tiketi 2,500 za Mashabiki wenye Tiketi za Msimu mzima zimerudishwa kwa ajili ya Mechi yao ya Alhamisi Usiku ya Ligi dhidi ya West Brom na sasa wanatafutwa Wanunuzi wapya.
Kitendo hicho ni wazi Mashabiki wamechukizwa na mwendo wa Arsenal.
Lakini Wenger, ambae Mkataba wake unakwisha Mei 2017, hakuyumbishwa na msimamo huo wa Washabiki na pia kusisitiza yeye atabaki hapo hapo Arsenal akitimiza Mkataba wake.
Wenger amedai: “Naheshimu Mkataba wangu!’
Katika Miezi ya hivi karibuni, Bango kubwa linalomtaka Wenger ang’oke Arsenal limekuwa litundikwa juu kwenye Mechi za Arsenal.
Wenger amesisitiza ni uamuzi wa Mashabiki wenyewe kwa hiari yao kuhudhuria Mechi za Arsenal Uwanjani Emirates ambako wameshinda Mechi 2 tu za Ligi tangu Februari.

Wenger ameeleza: “Tizama, kila mtu yuko huru kuamua nini anafanya kwa Tiketi yake ya Msimu. Ni Mechi ya Alhamisi Usiku na hii si kawaida. Pia hatukupata matokeo mazuri Mechi iliyopita Nyumbani na pengine hiyo ni sababu! Lazima tuishi na hayo!”