Thursday, April 21, 2016

MENEJA ENGLAND HODGSON AMTETEA JAMIE VARDY AKIDAI HAKUSTAHILI KADI NYEKUNDU!

Meneja wa England Roy Hodgson amejitumbukiza kwenye mjadala mkali unaovuma Nchini humo kwa kudai Straika wa Leicester City Jamie Vardy hakupaswa kupewa Kadi Nyekundu Jumapili iliyopita Leicester ilipotoka 2-2 na West Ham.
Katika Mechi hiyo Vardy alionyeshwa Kadi ya Njano ya pili na Refa Jon Moss kwa madai ya kujiangusha ndani ya Penati boksi na hivyo kutolewa nje kwa Kadi Nyekundu.
Vardy, mwenye Miaka 29 na ambae ameichezea England mara 6 chini ya Hodgson, amefungiwa Mechi 1 kwa Kadi hiyo.
Lakini huenda akafungiwa zaidi baada ya FA ya England kuamua kumfungulia Mashitaka ya Utovu wa Nidhamu kutokana na kumvaa Refa Moss kwa maneno makali mara baada ya kutolewa.
Hodgson amelivaa sakata hilo na kudai Vardy hakujiangusha kwa makusudi bali alikosa balansi kutokana na spidi yake kali.
Hodgson ameeleza: "Nadhani Beki wa West Ham (Angelo Ogbonna) alimgusa kidogo na kutokana na spidi yake kali alikosa balansi!"

Vardy, ambae amewafungia Vinara wa Ligi Kuu England Leicester Bao 22 Msimu huu, sasa anaweza kuzikosa Mechi zaidi ya ile na Swansea lakini Hodgson amezidi kumtetea: "Vardy alifanya kama vile binadamu mwingine angetenda katika mazingira yale. Tuelewe hilo!"