Tuesday, April 12, 2016

UEFA CHAMPIONS LEAGUE: LEO JUMANNE CITY v PSG, REAL MADRID v WOLFSBURG

UEFA CHAMPIONS LIGI
ROBO FAINALI

Marudiano Saa 3 Dakika 45 Usiku

Jumanne Aprili 12
Manchester City v Paris St-Germain [2-2]
Real Madrid v Wolfsburg [0-2]

Jumatano Aprili 13
Benfica v Bayern Munich [0-1]
Atletico Madrid v Barcelona [1-2] 

WAKATI MANCHESTER CITY wakiyumba kwa kumkosa Kepteni wao Vincent Kompany, Real Madrid wameimarika baada ya Straika wao Karim Benzema kupasishwa fiti kucheza Mechi ya Marudiano ya Robo Fainali ya UCL, UEFA CHAMPIONS LIGI Jumanne Usiku.
Man City watatinga Uwanjani kwao Etihad, Jijini Manchester kuivaa Paris St-Germain huku Timu hizo zikiwa Sare ya 2-2 baada ya Mechi ya kwanza na Meneja wa City, Manuel Pellegrini, kudai Kepteni wake Kompany hayuko fiti kwa Asilimia 100 kucheza Mechi hii.

Sentahafu Kompany, mwenye Miaka 30, hajaichezea City tangu watoke 0-0 na Dynamo Kiev kwenye Raundi iliyopita ya Mashindano haya iliyochezwa Mwezi Machi akisumbuliwa na tatizo lake sugu la Musuli za Mguu za nyuma ya Ugoko ambalo sasa limemkumba mara 14 tangu ajiunge na City Mwaka 2008.
City wanatarajiwa kuitumia kombineshini ile ile ya Masentahafu, Nicolas Otamendi na Eliaquim Mangala, waliocheza Mechi ya kwanza huko Parc des Princes Jijini Paris na kutoka 2-2 na PSG.

HUKO Santiago Bernabeu, ambako Real Madrid wako kwenye kauli mbiu ‘REMONTADA’ ikimaanisha kutoka nyuma na kupindua kipigo, wako kwenye kibarua kigumu cha kugeuza kichapo cha 2-0 toka VfL Wolfsburg walichopewa Wiki iliyopita lakini matumaini makubwa kwao ni kupona kwa Straika wao Karim Benzema.

Benzema aliumia Goti Wiki iliyopita kwenye kipigo hicho cha Wolfsburg na kulazimika kutoka nje mapema na pia kuikosa Mechi ya Real ya Jumamosi walipoitwanga Eibar 4-0.
Sasa Benzema yuko fiti kuungana na Safu ya Real ya mashambulizi wakiwamo Cristiano Ronaldo na Gareth Bale huku Kocha wao Mkuu, Lejendari Zinedine Zidane, akiishauri Timu yake kutumia akili zaidi, kujituma zaidi na kupigania kila Mpira ili wazoe ushindi.