Friday, April 29, 2016

VAN GAAL AJIGAMBA DHIDI YA LEICESTER CITY JUMAPILI, AWAAMBIA WASITEGEMEE USHINDI KIULAINI!

LOUIS VAN GAAL ameionya Leicester City kwamba Wachezaji wa Manchester United hawatawaruhusu kutwaa Taji la Barclays Premier League, BPL, Ligi Kuu England, Uwanjani Old Trafford hapo Jumapili wakati Timu hizi zitakapokutana.
Leicester, chini ya Kocha kutoka Italy Claudio Ranieri, wanahitaji Pointi 3 tu kutwaa Ubingwa wao wa kwanza wa England katika Historia ya Miaka 132.
Lakini Man United, wakiwa wamebakiza Mechi 4 za BPL, bado wamo kwenye vita ya kuwania kutinga 4 Bora ili wacheze UEFA CHAMPIONZ LIGI Msimu ujao.

Akiongea na Wanahabari hii Leo huko Aon Training Complex, Kituo cha Mazoezi cha Carrington Jijini Manchester, Van Gaal amesema: “Inabidi tuwafunge Leicester ili tubaki mbio za 4 Bora, lazima tuwafunge. Hatuwezi kuruhusu wawe Mabingwa Old Trafford. Nadhani watakuwa Mabingwa Wiki ijayo kwa hiyo hatutawaharibia Pati yao bali kuiahirisha tu!”

Man United v Leicester City KUKUTANA:

-Man United wamefungwa Mechi 1 tu kati ya 13 za mwisho dhidi ya Leicester na hiyo ilikuwa 5-3 Msimu uliopita huko King Power Stadium.
-Mechi ya mwisho kati ya Leicester na Man United ilichezwa Novemba 28 huko King Power Stadium na kuisha 1-1.
-Leicester, ambao wako kileleni mwa BPL kwa Siku zaidi ya 100, wamefungwa Mechi 1 tu kati ya 13 zilizopita.


Mbali ya kusema Ranieri na Leicester wanastahili Ubingwa, pia Van Gaal alieleza kuwa hilo ni jambo jema kwa England na Soka kwamba si Timu ile ile tu inatwaa Ubingwa.

Van Gaal ametamka: “Walipata nafasi ya kuchezesha Kikosi kilekile kwa vile hawakuwa na Mechi nyingi ukilinganisha na Timu nyingine. Ni jambo jema kwa Ligi Kuu na Soka kwamba si Timu ile ile tu inatwaa Ubingwa siku zote!”