Wednesday, April 13, 2016

VAN GAAL LEO KUUNGA UNGA SIKU! FA CUP MAUDIANO LEO DHIDI YA WEST HAM KUAMUA

Manchester United wamekuwa na Msimu mbovu mno na kila mara wakiyumba basi mwisho wa Meneja wao Louis van Gaal hutangazwa lakini kila mara Mdachi huyo huipanchi ‘Siku ya Hukumu’ yake.
Wadadisi na Wachambuzi huko England wamesema kila Man United ikifungwa, huku kila Mtu akitabiri Meneja huyo atatimuliwa, basi huja na matokeo ya kuwakonga nyoyo Mashabiki na Wapinzani wake wote ndani ya Man United.
Baada ya kutandikwa 3-0 na Arsenal huko Emirates Mwezi Oktoba kwenye BPL, Ligi Kuu England, Van Gaal akaiongoza Man United kuinyuka Everton 3-0 ndani ya Goodison Park kwenye Mechi ambayo hata Wachambuzi na wapinzani wake wakubwa walitingisha vichwa na kuungama Man United ilisakata Soka tamu mno.

Vikaja vipondo vinne mfululizo mikononi mwa Wolfsburg, Bournemouth, Norwich na Stoke lakini ikafuata Sare ya kuridhisha dhidi ya Mabingwa Chelsea.
Baada ya hapo vikaja vipigo viwili mfululizo toka kwa Sunderland na FC Midtjylland lakini tena ukaja ushindi murua dhidi ya Arsenal ndani ya Old Trafford.
Walipopigwa na Liverpool huko Anfield na kufuatia Sare Old Trafford iliyowatupa nje ya UEFA EUROPA LIGI, ukaja ushindi wa furaha kubwa kwa Mashabiki baada ya kuwatwanga Mahasimu wao wakuu Man City, tena wakiwa kwao Etihad, na kufufua matumaini mapya.
Hii Listi ya ‘Uma, Puliza’ haina mwisho.
Ukiondoa Mechi ya Marudiano ya FA CUP itakayochezwa Upton Park Jumatano Aprili 13 na West Ham, kwenye BPL, Ligi Kuu England, mpinzani anaefuata kwa Man United baada ya kutandikwa 3-0 na Tottenham Jumapili iliyopita, ni ‘kibonde’ Aston Villa Uwanjani Old Trafford.
Aston Villa yupo mkiani mwa Ligi na ni ‘tayari’ ashashuka Daraja na ni juu ya Man United kupiga msumari wa mwisho kwa Timu ambayo haijashinda Ugenini tangu waliposhinda Siku ya kwanza ya Ligi walipoipiga Crystal Palace ambao nao hawana ushindi tangu Desemba.
Hii ni nafasi nyingine murua kwa Van Gaal kuahirisha ‘Siku ya Hukumu’ yake.
Uamuzi wa nini hatima ya Van Gaal upo mikononi mwa Ed Woodward, Mkurugenzi Mtendaji, na Familia ya Glazer ambao ndio Wamiliki wa Man United.

Ukifuata historia ya hivi karibuni pale Mwaka 2014 David Moyes alipotimuliwa Miezi 10 tu ndani ya Mkataba wake wa Miaka 6 mara tu baada ya kufungwa 2-0 na Everton na hivyo kumaliza matumaini ya kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI, basi hilo linaweza kumkuta Van Gaal katika Mechi 3 zijazo ikiwa watazipoteza na City, ambao wako Nafasi ya 4, kushinda Mechi zao.
Hata hivyo, kufuatana na wapinzani wa Man United waliobaki, yaani Aston Villa, Crystal Palace, Leicester, Norwich, West Ham na Bournemouth, Wachambuzi wanahisi, kwa mara nyingine tena, Van Gaal ataahirisha ‘Siku ya Hukumu’ yake hadi mwishoni mwa Msimu.