Saturday, May 14, 2016

ED WOODWARD KIMYA KUHUSU MENEJA LOUIS VAN GAAL, WADAU WASHANGAA!

Van Gaal anaondoka au?Makamu Mwenyeki Mtendaji  wa Manchester United Ed Woodward hakutamka hata mara moja Jina la Meneja wao Louis van Gaal wakati wa Mkutano Laivu Mtandaoni na Wawekezaji wa Klabu hiyo na hilo limetafsiriwa na Wachambuzi kuwa mwisho wa Mdachi huyo umetimia.
Kwenye Mkutano huo, Woodward aliwasilisha Ripoti iliyoonyesha Man United imevuna zaidi ya Pauni Milioni 500 kama Mapato kwa Mwaka mmoja wakiwa wamekusanya Pauni Milioni 123.4, ongezeko la Asilimia 29.9, kwa Kipindi cha Tatu cha Mwaka 2016.

Wakiwa hatarini kukosa kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI, Msimu ujao ikiwa ni mara ya pili ndani ya Misimu Mitatu, Woodward aligusia nia yao kuwekeza Fedha za kutosha kununua Wachezaji wapya lakini hakumtaja Meneja Van Gaal hata mara moja.

Jambo hilo limetoa ishara kubwa kuwa Van Gaal huenda akatimuliwa mwishoni mwa Msimu huu ikiwa Man United wataikosa 4 Bora ambayo itawaruhusu kucheza UCL Msimu ujao.
Hivi sasa Man United wapo Nafasi ya 5 kwenye Ligi Kuu England wakiwa Pointi 2 nyuma ya Mahasimu wao Man City na ili kuikwaa Nafasi ya 4 Man United inabidi waifunge Bournemouth kwenye Mechi yao ya mwisho ya Ligi Uwanjani old Trafford hapo Jumapili na hapo hapo kuombea City wafungwe Ugenini na Swansea City.