Sunday, May 22, 2016

ENGLAND UWANJANI LEO DHIDI YA TURKEY KUJIANDAA NA EURO 2016 BILA MASTAA KADHAA!

JUMAPILI ni nafasi safi kwa Straika wa Tottenham Hotspur Harry Kane na yule wa Mabingwa Leicester City Jamie Vardy kuichezea England itakapoivaa Turkey Jumapili kwenye Mechi ya Kirafiki.
Mechi hii ni moja ya Mechi 3 ambazo England wameziandaa kabla kuanza kucheza Fainali za Mataifa ya Ulaya EURO 2016 Mwezi ujao.
Kane na Vardy Msimu huu wameng’ara mno kwenye Ligi Kuu England ambapo Kane alizoa Buti ya Dhahabu kwa kuwa Mfungaji Bora akiwa na Bao 25 moja zaidi ya Vardy ambae ndie alieibeba mno Leicester kutwaa Ubingwa.
Mastraika hao Wawili wameichezea pamoja England mara tu pale Mwezi Oktoba England ilipoinyuka Lithuania 3-0.
Kwa vile Kesho Mastraika wengine wa England, Wayne Rooney na Marcus Rashford, hawatacheza kutokana na kuichezea Klabu yao Man United Leo kwenye Fainali ya FA CUP na Daniel Sturridge kupumzishwa baada ya kuichezea Liverpool ya EUROPA LIGI hapo Jumatano, Kane na Vardy wataanza Mechi hii na Turkey itakayochezwa Jijini Manchester Uwanja wa Etihad.

Meneja wa England Roy Hodgson anatarajiwa kutumia Mfumo wa Mastraika Wawili mbele kwenye EURO 2016 ambao ni Kane na Vardy huku Kepteni wao Rooney akishuka kucheza nyuma yao kwenye Kiungo.
Turkey wanajipima kwa ajili ya EURO 2016 yakiwa ni Mashindano yao ya kwanza makubwa tangu wafike Nusu Fainali ya EURO 2008 baada ya kushindwa kufuzu Fainali za EURO 2012 na pia Fainali mbili zilizopita za Kombe la Dunia.
Turkey, chini ya Meneja Fatih Terim, kwenye EURO 2016 wapo Kundi D ambalo ni gumu pamoja na Mabingwa Watetezi Spain, Croatia na Czech Republic.

Mvuto kwenye Mechi hii ya Jumapili kwa upande wa Turkey ni uwezekano wa wao kumchezesha kwa mara ya kwanza Kinda wa Miaka 18 wa Klabu ya Denmark FC Nordsjaelland, Emre Mor, ambae alizaliwa Denmark lakini ameamua kuichezea Nchi ya asili ya Wazazi wake.