Friday, May 20, 2016

FAINALI EUROPA, KLOPP ADAI MAAMUZI MANNE YA REFA YALIWAUA NA KUAMBULIA KIPIGO!

MENEJA wa Liverpool Jurgen Klopp amedai yapo Maamuzi Manne ya Refa yaliyochangia wao kufungwa 3-1 na Sevilla kwenye Fainali ya UEFA EUROPA LIGI.
Kwenye Fainali hiyo iliyochezwa Jana huko St Jakob-Park, Basel Nchini Uswisi, Liverpool walitangulia kufunga kwa Bao la Kipindi cha Kwanza la Daniel Sturridge huku pia Refa kutoka Sweden Jonas Eriksson akiwaminya Penati 3 katika Kipindi hichohicho.
Pia Refa huyo aliupangua uamuzi wa Mshika Kibendera wake wa kuashiria Ofsaidi wakati Coke akiifungia Sevilla Bao lao la 3.
Klopp amedai bahati haikuwa yao na kueleza: "Leo kulikuwa na maamuzi manne ya wazi tuliyominywa. Ni Fainali na Mechi ni ngumu, unahitaji bahati na hatukuwa nayo. Kama ingekuwa 2-0 Haftaimu ingekuwa mambo mengine!"
Mjerumani huyo amekiri kuvunjika moyo kwa sasa lakini amesema kutocheza Ulaya Msimu ujao kutawapa muda mwingi wa mazoezi na hivyo kufanya vizuri kwenye Ligi na Mashindano mengine.
Kushindwa Jana kumemfanya Klopp awe amepoteza mfululizo Fainali 5 zilizopita na hiyo ni ya pili mfululizo akiwa Meneja wa Liverpool baada ya pia Mwezi Februari kubwagwa na Man City kwenye Fainali ya Capital One Cup.
Klopp amenena: "Sidhani kama Mungu ana mpango na mimi kwamba daima nipigwe tu Fainali. Sidhani kama mimi ni Mtu nisie na bahati Maishani!"