Tuesday, May 24, 2016

JOSE MOURINHO KUONEKANA LEO OLD TRAFFORD?

Baada ya hekaheka za Siku nzima iliyopambwa na kuvuja kwa habari zisizothibitishwa kuwa Louis van Gaal ametimuliwa kama Meneja wa Manchester United hatimae mambo yakawekwa rasmi hadharani.

Hapo Jana, Van Gaal aliwasili Kituo cha Mazoezi cha Carrington cha Man United Jijini Manchester mapema Asubuhi na kushinda huko kutwa nzima na kuondoka kabla ya Saa 11 Jioni huku habari zikivuja na kutapakaa Dunia nzima kutimuliwa kwake akiwa amebakiza Mwaka Mmoja wa Mkataba wake huku Jose Mourinho akitajwa kuwa ndie Mrithi wake lakini hakuna kitu rasmi kilichotangazwa kutwa nzima.

Lakini baadae Klabu ya Manchester United kupitia Makamu Mwenyekiti Mtendaji Ed Woodward ilitoa tamko rasmi na kuthibitisha kuondoka kwa Louis van Gaal kama Meneja huku nae Mdachi huyo akitoa tamko lake rasmi kuthibitisha hilo na kutoa shukrani.

Katika Taarifa yao, Man United, kupitia Ed Woodward, Mtendaji Mkuu huyo alisema: “Napenda kumshukuru Louis na Wafanyakazi wake kwa kazi njema waliyofanya kwa Miaka Miwili iliyopita waliyomalizia kwa kuifikia Rekodi ya kutwaa FA CUP mara 12 [Na kumfanya aweze kutwaa Taji katika Nchi 4 tofauti]. Amekuwa Mtu mwadilifu na wa heshima katika wakati wote aliokuwa hapa. Ametuachia urithi mkubwa na hasa wa kuwapa Vijana wengi fursa ya kuonyesha vipaji vyao katika jukwaa la juu kabisa. Kila Mtu toka Klabu hii anamtakia kila la heri katika maisha yake ya baadae.”
Tamko hilo lilimalizia kwa kutaja kuwa Mrithi wa Meneja atatangazwa haraka iwezekanavyo.
Nae Van Gaal alitoa tamko lake rasmi ambapo alisema ilikuwa heshima kubwa kwake kuitumikia Klabu kubwa kama Manchester United lakini akataja kusikitishwa kwake kwa kutoweza kukamilisha Miaka Mitatu ya Mkataba wake.

Lakini Van Gaal alisisitiza mafanikio yake na hasa kutwaa FA CUP ambayo anatarajia Msimu ujao yataisukuma Man United kupata mafanikio makubwa zaidi.
Pia aliwashukuru Mashabiki, Wasaidizi wake na Wachezaji na kutaja kufarijika sana na kuona Chipukizi wengi wakipata fursa na kuwatakia mafanikio makubwa zaidi huko mbeleni.

Mwishowe Van Gaal alitoa shukrani za dhati kwa Malejendari wa Manchester United Sir Alex Ferguson na Sir Bobby Charlton kwa kumfanya yeye na Familia yake wajisikie vyema katika muda wake wote kama Meneja wa Manchester United.
Ingawa Man United haijasema waziwazi lakini inaaminika Leo mazungumzo kati ya Ed Woodward na Wakala Jorge Mendes, anaemwakilisha Jose Mourinho, yatakamilika hii hii Leo na Mourinho kutangazwa kuwa ndie Mrithi wa Van Gaal.

Mourinho, Raia wa Ureno mwenye Miaka 53, amekuwa hana kibarua tangu aondoke Chelsea Mwezi Desemba ikiwa ni Miezi 7 tu tangu aipe Ubingwa wa England ukiwa ni Ubingwa wa 3 katika himaya zake 2 hapo Chelsea.

Pamoja na Va Gaal, Makocha Wasaidizi wake wote aliokuja nao inaaminika nao wataondoka lakini zipo habari ambazo hazijathibitishwa kuwa Meneja Msaidizi, Ryan Giggs, aliedumu Man United kwa Miaka 29, amepewa Ofa ya kubakia Klabuni hapo kwa wadhifa ambao nao haujulikani.
Ryan Giggs baada ya Kufukuzwa Meneja Van Gaal inawezekana nae Giggs Kaondoshwa au akabaki Old Trafford