Monday, May 16, 2016

MAN UNITED vs BOURNEMOUTH SASA KUCHEZWA KESHO JUMANNE, MASHABIKI KURUDISHIWA FEDHA KUINGIA BURE!

MECHI kati ya Manchester United na Bournemuth ya BPL, Ligi Kuu England, iliyokuwa ichezwe Jana Uwanjani Old Trafford na kufutwa Dakika za mwisho kabla kuanza kutokana na kugundulika Kifurushi chenye kutia wasiwai kwamba ni Bomu sasa itachezwa Jumanne Usiku Mei 17 kuanzia Saa 4 Usiku, Saa za Bongo.
Kwa mujibu wa ripoti za Polisi, Kifurushi hicho kiligundulika kwenye Choo cha Jukwaa la Stretford End na mwonekano wake ulikuwa ni kama Bomu na hivyo kuwalazimu kuchukua tahadhari kuwatoa Mashabiki wote waliokuwa kwenye Jukwaa hilo na lile la Sir Alex Ferguson na kisha kuamua kufuta Mechi hiyo na kuwatoa Mashabiki wengine wote Uwanjani hapo huku Uwanja mzima ukisachiwa.
Polisi wakalazimika kuita Kikosi Maalum cha Jeshi cha Kutegua Mabomu na Kikosi hicho kilifanikiwa kukilipua Kifurushi hicho ambacho baada ya uchunguzi kiligundulika ni Kifaa cha Mfano wa Bomu ambacho hutumika kwa Mazoezi ya Kiusalama na kuwa kilisahaulika na Kampuni ya Usalama iliyofanya Mazoezi ya Usalama Uwanjani Old Trafford Jumatano iliyopita.

Uongozi wa Man United, wakishirikiana na ule wa Bournemouth pamoja na BPL, wameamua Mechi hii kuchezwa Jumanne Usiku na Klabu ya Man United imeamua Mashabiki wote waliokuwa na Tiketi ya Mechi ya Jumapili iliyofutwa watarudishiwa Fedha zao na sasa kuingia Bure Jumanne Usiku.
Uamuzi huu utaigharimu Man United kiasi cha Pauni Milioni 3.
Mechi hii ni ya kukamilisha Ratiba tu kwani Bournemouth wako salama na hawagombei nafasi yeyote kucheza Ulaya ingawa kwa Man United ipo nafasi finyu ya kuipiku Man City toka Nafasi ya 4 na wao kucheza UCL, UEFA CHAMPIONS LIGI
lakini wanapaswa kuifunga Bournemouth Bao 19-0 ili kuipikua City ambao Jana walitoka 1-1 na Swansea City huko Liberty Stadium.
Kwenye Mechi hiyo City walitangulia kufunga Dakika ya 5 kwa Bao la Kelechi Iheanacho na Swansea kurudisha Dakika ya 46 kwa Bao la Andre Ayew.