Wednesday, May 11, 2016

RAIS TFF AIPONGEZA YANGA, BODI YA LIGI YAFAFANUA YANGA KUCHEZA NA NDANDA DAR!

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi ameipongeza timu ya soka ya Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.
Hii ni mara ya 26 kwa Young Africans ambayo kwa sasa inacheza mashindano ya kuwania kutwaa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kutwaa taji hilo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965. Simba inafuatia katika rekodi hiyo baada ya kulitwaa taji hilo kwa mara 18.

“Nichukue nafasi hii kuipongeza Young Africans kwa ubingwa. Pia nizipongeze timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya msimu wa Ligi Kuu Bara ya Vodacom 2015/16 kuwa wenye mafanikio,” amesema Rais Malinzi baada ya Young Africans kufikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo.
Kadhalika Rais Malinzi amezikumbusha na kuhamamisha klabu zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2016/17 kutoa maoni, mapendekezo, marekebisho ya ili kuboresha kanuni za uendeshaji wa ligi hiyo kwa msimu ujao. Maoni hayo yapelekwe kwa njia ya maandishi moja kwa moja kwenye ofisi za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) au kwa njia ya barua pepe tplb.tplb@yahoo.com

Young Africans imefikia rekodi hiyo baada ya kutwaa ubingwa katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992,1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006 na misimu ya 2007-2008, 2008-2009, 2010-2011, 2012-2013, 2014-15 na 2015-16.

Pamoja na kutangazwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2015/2016, kikosi cha timu ya Young Africans kwa sasa kimebakiza michezo miwili ambayo ni dhidi ya Ndanda unaotarajiwa kupigwa Jumamosi Mei 14, 2016 kadhalika dhidi ya Majimaji Mei 22 ambayo itakuwa ni siku ya kufunga pazia la Ligi Kuu msimu huu wa 2015/16.

NDANDA, YANGA KUPIGWA DAR MEI 14
Mpaka sasa taarifa kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Ndanda na Young Africans umepangwa kufanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mara baada ya Yanga kuomba hivyo na Ndanda kama timu mwenyeji kuridhia kuuhamisha kutoka Nangwanda Sijaona wa Mtwara.

Kwa nyakati tofauti, mwishoni mwa wiki iliyopita Young Africans ilituma maombi kwa Ndanda kadhalika TPLB kuomba ridhaa ya mchezo huo kufanyika Dar es Salaam kwa kuwa inatarajiwa kusafiri Jumapili alfajili kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidia ya Sagrada Esperanca ya Angola.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TPLB, Ndanda imekubali ombi la Young Africans iliyoomba mchezo huo uhamishwe kwa malengo ya kuisaidia Young Africans kuwahi usafiri ndege kwenda Angola ambako wanatarajiwa kucheza na wapinzani wao ama Mei 17 au 18, mwaka huu.

Barua ya Bodi ya Ligi kwa TFF imesema kwamba Young Africans watatumia mchezo huo ambao Ndanda itakuwa mwenyeji kupokea taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro ameishukuru Ndanda kwa uungwana wao wa kujali maslahi ya taifa na kukubali mchezo huo kufanyika Dar es Salaam, kabla ya Young Africans kwenda Angola.

Kanuni ya pili ya Ligi Kuu Bara toleo la 2015/16 imeeleza wazi kuwa, “Katika mazingira maalumu, timu inaweza kucheza mchezo wake wa nyumbani katika uwanja mwingine endapo kuna sababu nzito na za msingi, utambulisho wa uwanja katika mazingira haya pia unawajibika kufanywa katika kipindi cha uthibitisho wa kushiriki ligi au kwa maombi maalumu kwa TPLB,” inasehemu kanuni hiyo.
Kwa kuzingatia kanuni hiyo na sababu za Yanga ambazo Ndanda na Bodi wameona kuwa ni nzito wamekubaliana kucheza mchezo huo Dar es Salaam.
Yanga inatarajiwa kucheza na wapinzani wao, Sagrada Esperanca ya Angola ama Mei 17 au 18, 2016. Katika mchezo wa kwanza ulifanyika Dar es Salaam Jumamosi iliyopita Yanga iliwafunga wageni wake mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga inahitaji ama sare, ushindi na kama kufungwa basi si zaidi ya bao moja ili kuindoa Esperanca katika hatua ya awali, ili kuingia hatua ya makundi katika kusonga mbele.